*Mafuriko yasababisha kifo, wananchi wakimbia makazi
*Mawasiliano Arusha, Karatu yakatika, eneo lageuka kisiwa
*Askari JWTZ wapelekwa eneo la tukio, vijana wapata ajira
Na Said Njuki, Monduli
WAKATI mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini, zikisababisha
maafa makubwa kwa wananchi na kuharibu miundombinu, Mji Mdogo wa Mto wa Mbu, katika Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha, jana ulikumbwa na mafuriko yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja, kukata mawasiliano ya barabara na wakazi wa eneo hilo kupoteza mali za mamilioni.
Mafuriko hayo yamelifanya eneo hilo lionekane kisiwa baada ya kipande cha barabara kilichopo Mto Kirurumo, kupasuka ambapo mawe yaliyoanguka kutoka milima ya Mbulumbulu, yaliziba barabara kuanzia alfajiri ya jana.
Wakizungumza na Majira jana, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema mvua hiyo ilianza kunyesha saa nane usiku na baada ya saa moja, familia nyingi zililazimika kukimbia makazi yao na kutelekeza mali.
“Ilipofika alfajiri, mawasiliano ya barabara kati ya Arusha na Karatu yalikatika na kuzuia zaidi ya magari 800, kutoka pande zote kukwama, tangu saa tisda usiku tupo nje, mali zote tumeziacha ndani, hali ni mbaya, hatujala wala hatujui kinachoendelea,” alisema Bi. Asia Issa.
Baadhi ya wasafiri ambao baadhi yao walikuwa na ahadi za kwenda kuwaona madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam pamoja na watalii, walikwama kuendelea na safari baaada ya kumaliza ziara zao katika maeneo ya Hifadhi ya Ziwa Manyara na Ngorongoro.
Abiria aliyekuwa akisafiri na basi la Kampuni ya Sai Baba yenye namba za usajili T 779 AVW, lililokuwa likitoka Karatu kwenda Dar es Salaaam, Bw. Hassan Juma, alisema walifika eneo hilo saa 12 asubuhi lakini walishindwa kuendelea na safari.
“Mafuriko yamekwamisha safari yetu, jambo la kusikitisha nilikuwa na ahadi ya kukutana na daktari wake leo Jijini Dar es Salaam, hadi sasa sijui hatma ya tiba yangu,” alisema Bw. Juma.
Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Magesa Mulongo ambaye aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, alifika eneo hilo mapema asubuhi na kushuhudia maafa yaliyotokana na mvua hiyo.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), iliahidi kupeleka greda ili kuondoa mawe na kufanya ukarabati wa miundombinu katika eneo hilo.
Bw. Mulongo alisema, makandarasi wakiongozwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), wapo katika eneo hilo wakikarabati iundombinu iliyoharibika.
Alisema zaidi ya askari 100 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zaidi ya 100, kutoka Kikosi cha Mbuni na timu ya madaktari toka Arusha na Wilaya ya Monduli, wamepelekwa eneo la tukio kutoa msaada kwa wananchi.
“Maafa ni makubwa, yamesababisha kukatika mawasiliano kati ya Arusha na Karatu, nawahakikishia Serikali inajipanga kunusuru hali hii haraka iwezenavyo,” alisema.
Aliongeza kuwa, hadi sasa mtu mmoja amefariki dunia ambaye ni mlinzi wa tangi la maji katika Hoteli ya Manyara Serena, Bw. Ndaete Kurudumu (40).
“Huyu marehemu alikumbwa na maji yaliyotoka eneo jirani la Mto Kirurumo na kupelekwa zaidi ya kilomita tano, mwili wake umeharibika vibaya kwa kupondwa na mawe makubwa,” alisema.
Taarifa kutoka eneo la tukio ambazo hazijathibitika rasmi zinasema kuwa, baadhi ya watu, taasisi na kampuni zimeanza kutoa misaada ya chakula kwa waathirika.
Baadhi ya vijana walionekana kunufaika na mafuriko hayo kwa kubeba abiria waliokuwa na kulipwa sh. 1,000.
No comments:
Post a Comment