09 November 2011

Dkt. Murray hatiani kwa kumuua Jackson

LOS ANGELES, Marekani

ALIYEKUWA daktari wa Marehemu Michael Jackson, Dkt. Conrad Murray amekutwa na hatia ya kumuua (Mfalme huyo wa pop) kwa kukusudia, jopo la majaji limehukumu mjini Los Angeles.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), jopo la majaji saba, wakiwemo wanawake watano iliwachukua siku mbili hadi kufikia maamuzi hayo.

Jackson alifariki dunia, Juni 25 2009 kutokana na kuzidisha dozi ya dawa zenye nguvu za nusu kaputi aina ya propofol, ambazo hutumika wakati wa upasuaji.

Murray mwenye umri wa miaka 58, sasa anaweza kupata adhabu ya kifungo cha hadi miaka minne na kupokwa leseni ya tiba.

Kulikuwa na hali ya huzuni katika chumba cha mahakama, wakati hukumu ikisomwa.

Mwandishi wa BBC, Peter Bowes alisema wakati hukumu ikisomwa watu waliokuwa mitaani walilipuka kwa shangwe, huku wengine wakipiga makofi na kushangilia.

Familia ya Jackson, iliyokuwa katika chumba cha mahakama, ilikuwa imetulia.

Latoya Jackson ambaye ni dada wa marehemu, aliliambia Shirika la Associated Press (AP) kuwa familia yao imefurahishwa na hukumu hiyo.

"Michael alikuwa akituangalia sisi," alisema.

Polisi walikuwa na kazi kubwa ya kulinda usalama, wakati mashabiki mwanamuziki huyo walipokuwa  wamekusanyika katika eneo la mahakama, baadhi walikuwa na simu na waandishi walikuwa wakirekodi  na kuandika kuhusu hukumu pamoja, ili kutuma habari kwenye mtandao.

Baadhi ya mashabiki walitokwa na mchozi, ambapo walipata faraja baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Jopo la majaji lilitumia muda wa pungufu ya siku moja na nusu, ili kutoa hukumu ya kumhusisha kuua kwa kukusudia Dkt. Murray.

Murray alikuwa ni mtu aliyeaminiwa na Michael na kumfanya kuwa daktari wake binafsi na ambaye alikuwa akimpatia dawa za nusu kaputi, ambazo zilikuwa zikimsaidia kupata usingizi.

Dkt. Murray atafikishwa mahakamini baada ya mwezi mmoja kusomewa hukumu yake, ambapo anaweza kuhukumiwa kifungo cha miezi minne jela.

Wakati wa kesi mawakili wa Dkt.  Murray walimtetea kuwa alikuwa na kawaida ya kutumia dawa za kupunguza maumivu mwenyewe, bila ya kufuata ushauri.

Dkt. Murray aliwekwa mahabusu baada ya kutiwa hatiani na hatapata dhamana, hadi itakaposomwa hukumu yake Novemba  29, mwaka huu.

Baada ya uamuzi, askari walimfunga pingu Dkt. Murray na kumpeleka mahabusu.

Jopo la majaji lilikuwa na Mmarekani mweusi mmoja, wazungu sita. Kesi ilisikilizwa kwa wiki sita, idadi ya mashahidi ilikuwa ni 49 na vielelezo zaidi ya 300 viliwasilishwa mahakamani

Michael Jackson, aliyekuwa kipenzi cha mashabiki alifariki mwaka 2009, wakati akijiandaa kufanya maonesho katika Uwanja wa O2 Arena London, Uingereza.

1 comment:

  1. Inasikitisha sana, kama kweli Dk. Murray alimpatia dawa ya kumzidishia Mungu anajua yote. Mahakama ndiyo yenye mamlaka kumhukumu mkosaji, inasikitisha. Ulale Mahali Pema Peponi Michael Jackson.

    ReplyDelete