Na Jumbe Ismailly, Singida
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), mkoani Singida kimempongeza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania bara, Kapteni mstaafu John Chiligati kwa kushiriki kikamilifu katika mbio za mwenge wa uhuru, uliomaliza mbio zake mkoani humo Oktoba 26 mwaka huu.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Katibu wa CCM mkoani humo, Bi. Naomi Kapambala, wakati akielezea mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika mbio hizo mkoani humo.
Bi. Kapambala pia alimpongeza Jimbo la Manyoni Magharibi Bw. John Lwanji (CCM) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa wa Halmashauri Kuu mkoani humo kwa kuacha vikao vya Bunge vya kamati ya kudumu na kushiriki mbio hizo.
“Mheshimiwa Lwanji baada ya kukamilisha mbio za mwenge katika Wilaya yake, alinijulisha kuwa ataendelea kuwepo jimboni ili aweze kushiriki Kikao cha Kamati za Madiwani ndio arudi Dar es Salaam kuhudhuria vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea,” alisema.
Licha ya Bi. Kapambala, kutoa pongezi kwa wabunge hao, alipotakiwa kueleza sababu za wabunge wengine wa chama hicho kutoshiriki mbio hizo alisema alikuwa na taarifa ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Bi. Marther Mlata, kuwa yupo nje ya nchi kwa matibabu.
“Wabunge wengine hawajanijulisha chochote, licha ya kuwatumia taarifa za kuwataka kutopuuzia shughuli hii muhimu, hata mimi mwenyewe nashindwa kufahamu nini kimesabbisha washindwe kushiriki, Bw. Chiligati licha ya kuwa na shughuli nyingi za kichama, ameweza kushiriki mbio hizo sasa inakuwaje wengine washindwe,” alisema.
Kwa upande wao, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), nao hawakuhudhuria mbio hizo ambazo zilifika katika Wilaya za Iramba na Manispaa ya Singida.
Wabunge wa CCM ambao hawakushiriki mbio ni Mbunge wa Singida Mjini, Bw. Mohamed Dewji na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Bw. Lazaro Nyalandu.
Wengine ni Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Katibu wa Fedha na Uchumi CCM Taifa, Bw. Lameck Nchemba Mwigulu, Mbunge wa Singida Magharibi, Bw. Mohamed Missanga na Mbunge wa Iramba Mashariki, Bi. Salome Mwambu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa vijiji vilivyopo Wilaya za Iramba, walisema kutoshiriki kwa wabunge hao katika mbio hizo huenda ni kutokana na kutoona umuhimu wake.
Mkazi wa Kijiji cha Misigiri, Bw. Makala Shamkoma, alitoa angalizo kwa chama hicho kutowapa uhuru wawakilishi hao kwa madaoi kuwa hali hiyo inaweza kukigharimu chama hicho.
“Kama wabunge hawa wangetakiwa kuja kuomba kura kwa wananchi wangeona umuhimu wa kuja lakini kwa sababu wameshapata uongozi, hawaone umuhimu wa kuwa karibu na wapiga kura wao,” alisema.
Wabunge wa CHADEMA ambao hawakuhudhuria mbio hizo ni Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tundu Mughwai Lissu na Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Christowaja Mtinda.
No comments:
Post a Comment