Na Peter Mwenda
WAUMINI wa Kanisa Katoliki Tanzania wametaja chanzo cha ajali za mara kwa mara katika eneo la Chalinze na Kibaha Mkoa wa
Pwani kuwa ni msongamano mkubwa wa magari huku kukiwa na barabara finyu.
Kutokana na hali hiyo wameitaka serikali kupanua barabara ya Morogoro kuanzina Dar es Salaam hadi Chalinze na kuanzishwa kwa Bandari kavu (ICD) eneo la Ruvu kama njia mojawapo ya kupunguza ajali za barabarani katika maeneo hayo.
Akizungumza kwa niaba ya waumini wenzake wa Kanisa hilo katika Ibada ya kuombea miili ya marehemu mapadre watatu waliokufa katika ajali gari eneo la Ruvu kwa Zoka Jumanne iliyopita, Mwenyekiti wa Walei Parokia ya Pugu, Bw. Joseph Selasini, alisema pamoja na hatua hiyo pia kianzishwe kikosi cha uokoaji ambacho kinasaidia kunasua majeruhi wa ajali.
Bw. Selasini ambaye pia ni ni Mbunge wa Rombo alisema ajali iliyouwa mapadre hao watatu na mtumishi wa Kanisa mmoja ingeweza kuepukika kama kasoro alizotaja zingeondolewa.
Katika ajali hiyo mapadre watatu Silverio Ghelli, Corrad Trivelli, Luciano Baffigi na mtumishi wa Kanisa Andrewe walikuwa baada ya gari waliyokuwa wakisafiria Toyota Land Cruiser hard Top namba T 903 ACQ kugongana uso kwa uso na lori.
"Marehemu Silvario Ghelli ambaye alikuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Pugu maisha yake yangeweza kuokolewa kwa sababu baada ya ajali alipiga kelele ya kuomba msaada wamnasue lakini baada ya saa moja na nusu ndipo alipokuja fundi gereji aliyemsaidia lakini tayari alikuwa amekufa," alisema Bw. Selasini.
Katika ibada hiyo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Benard Membe aliyewakilisha serikali alisema Rais Jakaya Kikwete, amepokea msiba huo kwa majonzi makubwa na kwamba serikali inatambua mchango mkubwa wa wamishionari hao katika maendeleo ya watanzania.
Bw.Membe alisema serikali inatambua mchango wa wamishionari hao katika sekta ya afya, elimu na sekta nyingine zinazogharamikiwa na Kanisa hivyo serikali inaungana na waumini wa Katoliki wa Tanzania na Italia kuombeleza vifo hvyo.
Awali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Policarp Kadinali Pengo, alisema vifo hivyo ni ishara wa waumini hao kukaa tayari kumtumikia Mungu kwa kutenda mema katika maisha yao ya duniani.
Askofu Pengo alisema Shirika la Wakapuchini limefanya kazi kubwa katika maendeleo ya tanzania kabla na baada ya uhuru hivyo vifo vya mapadre yao ni mbegu ya imani ya dhati.
No comments:
Post a Comment