Na Emmanuel Msigwa, Songea
MKOA wa Ruvuma upo kwenye mikakati ya kuwashawishi wawekezaji kujenga kiwanda cha sukari mkoani humo pamoja na kufufua
Kiwanda cha kusindika Tumbaku cha SAMCU kilichopo mjini Songea kilichofungwa tangu mwaka 2000.
Akizungumza katika Kikao Cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Ruvuma (RCC) mwishoni mwawiki, Mkuu wa Mkoa huo Bw. Said Mwambungu, alisema tayari ameshaanza kuzungumza na baadhi ya wawekezaji kujenga kiwanda hicho ili kuinua mkoa huo kiuchumi.
“Nimeshazungumza na kuwaomba baadhi ya watu kuja kuona uwezekano wa kujenga kiwanda cha sukari hapa kwetu na wiki ijayo wanakuja kufanya mzunguko wa angani kukagua, tukijengewa kiwanda cha sukari hapa kwa kweli tutakuwa mbali sana,” alisema Bw. Mwambungu.
Kuhusu Kiwanda cha kusindika Tumbaku cha SAMCU ambacho kilichokufa miaka 10 iliyopita, Mkuu huyo wa mkoa alisema amezungumza na Kampuni ya Demon ya Mororgoro ili kufufua kiwanda hicho na kuongeza ajira kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma.
“Tunaendelea kuwabembeleza ili wafufue kiwanda hiki cha SAMCU, kwa hiyo tukipata kiwanda cha sukari na hiki cha Tumbaku na barabara zetu zinazojengwa kwa kiwango cha lami zikikamilika kwa kweli hata wale wanasema Ruvuma ni mbali watavutika na kuja kwa wingi zaidi,” alisisitiza Bw. Mwambungu.
Alisema kufanikiwa kwa hatua hiyo ni fursa pekee kwa wawekezaji wa mahoteli kuwekeza katika sekta hiyo kwa kujenga hoteli makubwa kwa kuwa mkoa huo una changamoto kubwa ya kukosa vivutio hivyo vya kutosha.
Alisema serikali inaendelea kufungua milango kwa wawekezaji kujenga mahoteli mkoani humo na kuongeza idadi ya ndege kwenda Songea ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za nauli ya sh. 400,000 kwa safari moja kwenda Dar es Salaam.
Kwa upande wao wajumbe wa kikao hicho Bw. Oddo Mwisho na Bw. Charles Mhagama wakaguswa na tatizo kubwa la umeme wa uhakika huku wengine wakilalamikia gharama kubwa za kuingiza umeme huo majumbani mwao.
Walisema gharama za kuingiza umeme zimekuwa kubwa mno huku Shirika la ugavi wa umeme (TANESCO) likiwatoza wananchi nguzo moja ya umeme kiasi cha Sh. Milioni moja hali ambayo inatishia wananchi wa kawaida kushindwa kumudu gharama hizo.
Akizungumzia hali ya upatikanaji umeme Meneja TANESCO Mkoa wa Ruvuma, Bi. Monica Kebara, alisema ufungaji mashine aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete, mwaka 2009 alipofika mjini Songea umeshakamilika na kwamba hivi sasa upo katika hatua ya matazamio.
No comments:
Post a Comment