07 October 2011

Yanga yatembeza mkwara

*Wanaotumia nembo yao kukiona
Na Zahoro Mlanzi

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, umetoa notisi ya mwezi mmoja kuanzia jana kuhakikisha wafanyabiashara wanaouza kinyemela bidhaa zenye nembo yao
kujisalimisha kwao kabla ya Novemba, mwaka huu.

Bidhaa hizo ni shati, kofia, kalamu, jezi, miamvuli, soksi, kiwekea funguo na zinginezo ambazo huuzwa huku zikiwa na nembo ya Yanga.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Selestine Mwesiga alisema wanajua kuna bidhaa nyingi za Yanga ambazo zinauzwa bila ya wao kunufaika nazo.

"Tumeshafuata sheria zote zinazohusika, ambapo zoezi hilo la kamata kamata litaaza Novemba mwaka huu, hivyo wale wote  ambao huuza bidhaa zetu bila ya sisi kunufaika nazo, tunaomba waje tuzungumze," alisema Mwesiga.

Alisema mpaka kupata hati miliki nembo yao kutoka kwa Brela iliwagharimu zaidi ya sh.milioni 10,kitu ambacho kilikuwa cha muda mrefu lakini ufuatiliaji haukuwa makini.

Katibu huyo alisema wanajua kuna wafanyabiashara bado wana makontena  yenye bidhaa hizo na hata baadhi ya maduka makubwa nchini ambapo kutokana na hilo wanaweza kuzungumza nao ili wamalizie mzigo waliokuwa nao.

Alisema safari hii wamepania kuhakikisha hilo linafanyika na litakuwa endelevu, ambapo baada ya kutoa tangazo hilo hawatakuwa na simile katika kuwachukulia hatua.

"Tumeingia mkataba na kampuni ya sheria ya Lex Global,tutakapoanza kazi hiyo ya kamata kamata, tutakuwa nao bega kwa bega," alisema Mwesiga.

No comments:

Post a Comment