03 October 2011

Watakiwa kuacha imani potofu chanjo ya polio

Na Timothy Itembe, Tarime

WANANCHI wilayani hapa wametakiwa kuondokana na imani potofu kuhusu kampeni ya chanjo ya polio inayoendeshwa na serikali kwa takriban siku nne katika Mkoa wa Mara kwa
lengo la kuwakinga watoto na ugonjwa huo hatari.

Wito huo ulitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime Bw. John Henjewele, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. John Tupa, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika mji mdogo wa Sirari wilayani hapa.
Kampeni hiyo inaendeshwa na serikali mkoani hapa kufuatia kuibuka kwa ugonjwa wa polio Kamagambo Rongo nchini Kenya hivyo kuhatarisha maisha ya watoto wa Mkoa wa Mara kutokana na mwingiliano wa mpakani kati ya nchi hizo mbili.

Bw. Henjewele alisema wananchi wa Tarime kwa ujumla wanapashwa kuondokana na imami potovu za kiitikadi kuwa kumchanja mtoto kinga ya ugonjwa wa polio ni kumsababishia ugumba wakati wa utu uzima.
Aliwataka wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kupatiwa chanjo hiyo katika vituo vilivyopendekezwa.

Pia alitoa wigo kwa wananchi wote kushirikiana na kuwafichua wote wanaoficha watoto wao kutopata chanjo hiyo wakati wa kampeni hiyo muhimu kwa manufaa ya taifa zima.
Alisema licha ya kampeni hiyo kuwalenga watoto wote waliochini ya umri wa miaka mitano pia inawalenga wale ambao hawakumaliza chanjo wakati wakiwa wachanga na ambao hawakupata huduma hiyo kabisa awali.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Mara Bw. Samsoni Winani, alisema atahakikisha wananchi wa mkoa huo wanajikinga kikamilifu na magonjwa mbalimbali na kupata huduma bora ya matibabu katika Hospitali zote za serikeli, mashirika ya Dini na watu binafsi.

Alisema serikali imechukua hatua za haraka madhubuti kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia sita ya watoto hawajakamilisha chanjo hiyo huku asilimia mbili wakiwa hawana kinga kamili ya chanjo ya ugonjwa wa polio katika Mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment