Na Raphael Okello, Serengeti
UONGOZI wa Mfuko wa hifadhi ya Grumeti katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti Mkoa wa Mara, umesema uhusiano wa karibu kati yao na viongozi wakiwemo wale wa taifa
kutembelea na kuhifadhiwa katika Hoteli za Kampuni hiyo inatokana na maombi wanayopata kutoka kwa viongozi hao.
Pia imesema uhusiano mzuri kati yao na viongozi hao haulengi kupata upendeleo kutoka serikalini kwa lengo la kunyonya rasilimali ya Watanzania.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Singita Grumeti Fund Bw.Brian Harris, alisema ziara ya nyingi za viongozi wa kitaifa katika Hoteli hiyo zinatokana na maombi ya viongozi hao na kwamba yeye kama Mwekezaji anaonesha ukubali baada ya yeye kupata maombi.
“Kuna madai kuwa Grumeti imekuwa ikiwaalika viongozi wakuu wa serikali kufika hotelini hapa ili kampuni ipate upendeleo wa kutumia vibaya rasilimali ya nchi hii na kuwanyanyasa raia.
Ujio wa viongozi hao inatokana na maombi ya baadhi ya viongozi wa serikali ambao wanatuomba tuwaruhusu kutembelea Hoteli zetu,” alisema Bw.Harris na kuongeza “Hakuna siku sisi kama kampuni tumeandika barua kuomba viongozi wa serikali kuja kukaa hapa‚...hakuna, wala sisi hatujaomba kupata upendeleo kutoka kwa viongozi hao, sisi wakiomba tunawakaribisha kama viongozi wa serikali na kama wageni wengine,” alisisitiza Bw.Harris.
Alikanusha taarifa kwamba kampuni hiyo inapata faida kubwa kutokana na rasilimali ya uhifadhi hiyo ya Serengeti na kudai kuwa ni upotoshaji huku akiwaomba wananchi kuongeza ushirikiano zaidi kwa wawekezaji badala ya kuona kuwa ni maadui.
Alisema kuwepo kwa hoteli hizo za wawekezaji katika hifadhi ya Serengeti kunaipatia taifa fedha nyingi zinazotumika kwa shughuli za maendeleo.
Alisema fedha hizo zinatokana na hoteli hizo kuingiza watalii na kwamba malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuwa wawekezaji hawafanyi lolote kwa maendeleo yao inawavunja moyo wawekezaji kuja nchini.
Alisema wawekezaji wanachangia fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ya wananchi wanaozunguka hifadhi ya Grumeti katika Wilaya za Serengeti na Bunda lakini baadhi ya watumishi wa serikali hutumia vibaya fedha hizo hivyo kusababisha miradi mingi kukwama na mwekezaji kubaki kwenye lawama.
“Kila mwaka halmashauri zinakuja kuomba tuwasaidie kutekeleza miradi mbali mbali nasi tunakubali na kutoa fedha lakini miradi mingi inakwama mikononi mwao,” alisema Bw.Harris.
Aliwaomba viongozi wa serikali na jamii katika ngazi za vijiji kutowaona wawekezaji kama adui na wanyonyaji wa rasilimali zao badala yake waoneshe ushirikiano na kuwasilisha maoni yao na mapendekezo kwa njia ya amani badala ya kunung’unika.
Alivituhumu baadhi ya vyombo vya habari kujenga taswira mbaya kwa wawekezaji kuja nchini na kuwakatisha tamaa wale waliopo na kudai kuwa tabia hiyo inaweza kurudisha nyuma sifa nzuri ya Tanzania kwa wawekezaji.
Alisema baadhi ya wakurugenzi watendaji wa halmashauri zinazonguka hifadhi hiyo si wawazi kwa wananchi kuhusu miradi na misaada inayotolewa na Kampuni yake kwa wananchi na kwamba jambo hilo ndilo linalochangia wananchi kutowapenda wawekezaji.
Alisema hivi sasa hoteli ya hifadhi ya Grumeti katika hifadhi ya Serengeti imeshika nafasi ya kwanza katika Hoteli 100 bora duniani na kwamba hiyo ni sifa kwa Tanzania kuwavutia wawekezaji na watalii kuingia nchini na kukuza uchumi wa taifa.
No comments:
Post a Comment