05 October 2011

Kaya 80 zabomolewa nyumba Mwanza

Na Jovin Mihambi, Mwanza

ZAIDI ya kaya 80 katika Mtaa wa Ghana jijini Mwanza hazina mahali pa kuishi kutokana na Uongozi wa Halmashauri ya Jiji hilo kubomoa nyumba walizokuwa wanaishi
ili kupisha ujenzi wa mradi wa Jengo la Machinga(Machinga Complex).

Shughuli ya ubomoaji wa nyumba hizo ilianza jana saa 3.00 asubuhi, mwandishi Majira alilishuhudia tingatinga la halmashauri ya jiji aina ya Komatsu namba 40 likibomoa nyumba hizo.

Watu waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo walionekana wakihangaika huku na kule kuhamisha vifaa vyao kutoka katika nyumba hizo.

Mmoja wa wapangaji ambaye ameathiriwa katika shughuli hiyo, Bi. Bahati Shaaban alisema kuwa halmashauri ya jiji haikuwatendea haki kutokana na kuwapatia muda mfupi wa saa 24 kuwataka kuhama mara moja kutoka katika nyumba zao.

“Mimi nimechukia kwa jinsi ambavyo tumedhalilishwa hivi, jiji wanakuja kutudhalilisha walitupatia barua ya kututaka tuhame tukakubaliana nayo na notisi yao ilikuwa inaishia mwaka kesho mwezi wa pili.

"Walituahidi kuwa tungelipwa fidia, lakini ghafla wanakuja kutuhamisha kama utaratibu ndio huu kwa kweli mimi sitashiriki katika uchaguzi ujao, maana tunawachagua viongozi ili watusaidie,” alisema Bi. Shaaban.

Naye, Bw. Musa Joseph ambaye alikutwa akihamisha vyombo vyake kutoka katika moja ya nyumba hizo alisema kuwa shughuli hiyo imemuathiri kwa madai kuwa ameondolewa kutoka katika nyumba hiyo bila ya kupewa taarifa.

Alisema kuwa iwapo angepewa taarifa mapema angejiandaa ikiwa ni pamoja na kutafuta sehemu ya kuisitiri familia yake.

“Kweli tulipewa notisi ya muda mrefu na shauri la nyumba liko katika Mahakama ya Ardhi na Nyumba, kabla shauri hili
halijatolewa uamuzi na mahakama.

"Tunashtukia Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia mabango yake waliyoaandika kwenye kuta za nyumba, wanatutaka tuhame leo hii (jana) ndani ya saa 24, jamani kweli huu ni uungwana?’ alihoji Bw. Joseph.

Mkazi mwingine aliyeathirika na shughuli hiyo, Bw. Joseph Peter alisema kuwa halmashauri hiyo imefanya makosa ya kuwahamisha bila ya kufuata utaratibu jambo ambalo amesababisha waanze kutafuta makazi mengine hata kupanga katika vibanda vya mbwa kutokana na uhaba wa nyumba.

“Angalia sasa hivi ni kipindi cha mvua na inaweza ikanyesha wakati wowote, hatuna maturubai kwa ajili ya kujihifadhi kwa muda mimi na familia yangu, hivi unavyotuona ndivyo tulivyo na sijui tutakwenda
wapi na masika ndiyo haya yanakuja,” alisema.

Aliiomba serikali kuwapatia maturubai kwa ajili ya kujisitiri wakati wakiwa katika harakati ya kutafuta sehemu nyingine ya kupanga.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Bw. Wilson Kabwe alisema kuwa tayari notisi ya kuhama wakazi hao aliowaita kuwa ni wavamizi ilikwishatolewa kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita na kwamba kilichokuwa kinasubiriwa ni wao kuhama bila ya kubughudhiwa.

“Shughuli ya leo kuwahamisha wananchi hao ni ya kisheria, waliokuwa wanaishi hapo walipewa notisi ya kuhama na hao tunaowahamisha leo ni wavamizi na ndio maana tunawahamisha kwa sababu walikaidi kuhama,” alisema Bw. Kabwe.

Kwa mujibu wa Kabwe, alisema kuwa tayari usanifu wa mchoro kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Machinga  ulikwishafanyika na soko hilo linajengwa katika eneo hilo la Mtaa wa Ghana, Wilaya ya Ilemela.

Uchunguzi wa Majira umebaini kuwa watu hapa walipangishwa nyumba hizo kinyume cha sheria na ndugu na jamaa zao.

Nyumba hizo zilipangishwa kwa kiwango cha kati ya sh. 600,000 hadi sh. 2,000,000 kinyume na taratibu za upangaji.

1 comment: