Na Eckland Mwaffisi
WAKATI Serikali ikiwataka Watanzania kuunga mkono uchimbaji madini ya urani katika Hifadhi ya Taifa ya Selous, mkoani Ruvuma, baadhi ya
wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, wamehoji iweje Serikali itoe kibali cha utafiti wa madini hayo katika eneo la urithi wa dunia.
Wakizungumza na Majira Dar es Salaam juzi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walisema, hofu kubwa waliyonayo ni usiri uliopo katika taratibu za kuuibua mradi huo.
Utafiti wa madini hayo unafanywa na kampuni ya Mantra Tanzania Limited tangu mwaka 2007 na kuongeza kuwa, lipo tatizo la mgongano wa kisheria kati ya Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Maliasili na Utalii.
“Kuna mambo ambayo Wizara hizi hazijakubaliana juu ya kuanza kwa mradi huu mwaka 2014, wabunge tunahitaji kueleweshwa zaidi, usiri uliopo ni mkubwa, mara nyingi Watanzania hawanufaiki na madini yao, sasa tutasimama kidete,” walisema wajumbe hao.
Mwishoni mwa wiki, wajumbe wa kamati hiyo walitembelea eneo la utafiti wa madini hayo na baada ya kurejea Dar es Saalaam, Wizara ya Maliasili na Utalii iliandaa semina iliyojadili mchakato wa kuchimba madini hayo mwaka 2014.
Semina hiyo ilishirikisha wajumbe wa kamati hiyo, wadau wa mazingira, madini na wanahabari.
“Sisi wabunge tunapaswa kupewa maelezo ya kina ili kujua madini haya yatawanufaishaje Watanzania na wakazi wa Namtumbo, ndio maana wanaharakati wana wasiwasi mkubwa na mradi huu,” walisema.
Mwenyekiti wa kamati hiyo na mbunge wa Kahama, mkoani Shinyanga, Bw. James Lembeli, aliitaka Serikali kuona umuhimu wa kuifanyia marekebisho sheria ya madini.
“Sheria ya madini imekaa kimya ndio sababu inayochangia migogoro mingi katika sekta hii, nawaomba wanasheria muishauri Serikali ili sheria hizi ziweze kufanyiwa marekebisho,” alisema.
“Kuna kanuni nyingi zinahitaji kutungwa kwenda sanjari na utafiti na uchimbaji urani lakini lakini kanuni hizo hakuna,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Tabora, Bi. Magdalena Sakaya, alihoji kwa nini Serikali ilitoa kibali cha kufanya utafiti wa madini hayo wakati Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ambalo linahusika na uhifadhi wa maeneo ya kiutamaduni duniani halijatoa kibali.
Mbunge wa Namtumbo, Bw. Vita Kawawa, alitaka kujua wananchi wake watanufaikaje na mradi huo kwa mujibu wa kanuni za madini.
Watanzania tutafaidi madini yetu kama tu mikataba inayohusika itakuwa wazi na upedeleo wa makusudi kuwa taifa liwe na asilimia zenye manufaa kwa nchi siyo kupewa 3% wakati wahusika wameshapewa mabilioni kwenye acc zao nje ya nchi.Nigekuwa na uwezo investors wapewe 60% na sisi tubaki na 40% wakirudisha mutaji iwe nusu kwa nusu.HAWATAKI WAONDOKEserikali ianze kuwekeza kwenye elimu husika hivyo huko mbele tunakuwa na wataalamu wetu.
ReplyDelete