*Wachezaji kupewa 'fuba'
Na Zahoro Mlanzi
SIKU chache baada ya Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Timbe kusitishiwa mkataba wake na klabu hiyo, kocha mwenzake wa
timu ya Simba Mosses Basena, ameingiwa na wasiwasi kwamba huenda kikamkuta kama cha kocha huyo.
Mbali na hilo, Kamati za Simba zilizochaguliwa hivi karibuni, leo zinakwenda kutembelea kambi ya timu hiyo iliyopo Bamba Beach, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana na gazeti hili, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema kocha huyo amekuwa katika wakati mgumu tangu mwenzake Timbe, atimuliwe kwa kile kinachodaiwa kuna viongozi hawakuridhika na kiwango chake.
"Unajua Timbe alikuwa na rekodi nzuri Yanga, ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Chalenji, lakini cha kushangaza amesitishiwa mkataba, lakini yeye (Basena) ameipa Simba ubingwa wa Ngao ya Jamii, ndicho kitu kinachomuumiza kichwa.
"Hata ukiangalia kwa upande wa mashabiki na wanachama, asilimia kubwa hawaridhishwi na kiwango cha kocha huyo, licha ya kwamba mpaka sasa timu hiyo haijafungwa mechi yoyoye ya Ligi Kuu," alisema.
Alisema na pia mtihani mwingine kwa Basena, utakuwa Jumamosi ambapo watacheza na Yanga na akifungwa mchezo huo ndiyo atazidi kujiweka katika mazingira mabaya zaidi.
Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa klabu hiyo Ezekiel Kamwaga, alisema Wajumbe wa Kamati ndogo ndogo za klabu hiyo ambazo zimeboreshwa na Kamati ya Utendaji, leo wanakwenda kuzungumza na wachezaji wao waliopo kambini Bamba Beach.
Alisema zitakutana na wachezaji hao, ili kuwapa motisha kwa kuhakikisha mchezo dhidi ya Yanga wanaendeleza wimbi la ushindi na kutimiza azima yao ya kutopoteza mchezo wowote katika mzunguko wa kwanza.
"Kamati zote zilizoteuliwa na Kamati ya Utendaji, kesho (leo) zitakwenda kambini na kikubwa kwenda kuwapa motisha kwa kuwaahidi kuwapa chochote kitu, ili washinde mchezo huo," alisema Kamwaga.
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, alisema wachezaji wao wapo vizuri na wanaendelea na mazoezi kama kawaida na wote wapo katika morali nzuri.
Timbe ameikuta Yanga imeshacheza michezo karibu yote na imebakiwa na michezo mitatu kumaliza ligi ya bara hivyo haiingii akilini kumnadi eti ameipatia yanga ubingwa wa bara ni kwa mahesabu gani hapa yaliyo tumika?
ReplyDelete