26 October 2011

Timu ya taifa ya pool yatangazwa

Na Mwali Ibrahim

KOCHA mkuu wa timu ya taifa ya mchezo wa pool, Denis Lungu ametangaza vikosi viwili vya timu hiyo vitakavyoingia kambini
kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Mataifa ya Sfrika.

Mashindano hayo yanatarajia kufanyika Novemba 22 hadi 26 mwaka huu Jijini Blantyre, Malawi.

Kocha huyo aliwataja wachezaji hao kutoka katika Kundi A kuwa ni Omari Akida, Godfrey Mhando na Mohamed Idd wote kutoka Kinondoni, Felix Athanas wa Dodoma na Ally Akbar wa Temeke.

Aliwataja wa Kundi B kuwa ni Bonifance John wa Arusha, Baraka Joachim wa Mbeya, Jogory Makenzi wa Mwanza, Anthony Thomas na Hamis Nassoro wa Ilala na Ramadhani Ally wa Morogoro.

Wengine katika kundi hilo ni Emmanuel Loya wa Dodoma, Charles Venas wa Temeke, Abdallah Hussein wa Kinondoni na kutoka Manyara ni Emmanuel Sanka.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Lungu alisema kambi hiyo itaanza Oktoba 29, mwaka huu Dar es Salaam huku mashindano hayo yakitarajia kushirikisha nchi zote ambazo ni wanachama wa chama cha (AAPA).

Nchi hizo ni Afrika Kusini, Malawi, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Zambia, Uganda, Swaziland, Reunion FFB, Falme za nchi za Kiarabu, Nigeria, Msumbiji, Morocco na Lesotho.

Naye Meneja wa Bia ya Safari Lager ambao ndiyo wadhamini wa mchezo huo, Oscar Shelukindo alisema kampuni yake, imeamua kuidhamini timu hiyo kwa ajili ya kushiriki katika mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment