25 October 2011

Waziri kujieleza Kamati ya Bunge

*Ni kwa kushindwa kuteua Bodi Utalii
*Wajumbe bodi ya zamani watimuliwa
*Hesabu Benki ya Posta zakataliwa
*Mrema kumwona JK wizi halmashauri


Na Waandishi Wetu

KAMATI za Bunge zimeanza kukunjua makucha baada ya Kamati ya Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC) kumtaka Waziri kufika mbele yake kujieliza kuhusu mapungufu kadhaa, huku ikimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kurudia ukaguzi wa dharura wa sh. bilioni 1.1 zinazohisiwa kutoweka kifisadi.

Wakati hayo yakiendelea Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC) Bw. Augustino Mrema, ameijia juu serikali, akisema nchi iko hatarini kutokana wizi wa fedha za umma uliokithiri katika halmashauri za wilaya na kuahidi kuonana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete kuzungumzia tatizo hilo.

Kisa cha Waziri Maige

Katika kikao chake cha jana katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, Kamati ya Hesabu ya Mashiria ya Umma ilisema inamtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige kwenda mbele yake Oktoba 31, mwaka huu kujieliza sababu za kushindwa kuunda Bodi ya Utalii.

Akizungumza mbele ya kamati hiyo na viongozi wa Idara ya Utalii jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Zitto Kabwe alisema hawawezi kuendelea na mapitio ya matumizi ya wizara hiyo kwa kuwa hakuna bodi inayowajibika kujibu maswali yao, hasa iwapo kuna mapungufu ya mahesabu.

Alisema kamati yake inashangazwa na sekta ya utalii kufanya kazi bila ya kuwa na bodi huku ikikusudia kukuza utalii nchini na kumtaka Waziri Maige kufika siku hiyo bila kukosa kujibu maswali ya kamati.

"TANAPA walishaunda bodi, Ngorongoro walisaunda bodi, ninashangazwa na sekta hii ya utalii kutokuwa na bodi," alisema Bw. Kabwe.

Alisema idara ya utalii ilishatumia sh. bilioni 21 bila ya utaratibu jambo ambalo ni makosa na kwamba uenda kuna ubadhilifu mkubwa katika matumizi hayo kwa kuwa hakuna bodi inayowajibika kujibu hivyo kumtaka msajili wa hazina kutokutoa fedha zozote hadi hapo tatizo la idara hiyo litakapomalizika.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya mwaka 2008 ambayo ilimaliza muda wake Desemba mwaka jana na kuongezewa muda hadi Machi mwaka huu, Bw. George Lubeleje alikiri kuwa idara hiyo haina bodi na ni kosa kutokuwa na chombo hicho.

Bw. Lubeleje aliweka wazi kuwa bodi ilishamaliza muda wake na kuongeza na kwamba suala la bodi ni la waziri ndiye mwenye mamlaka.

"Rais anateua mwenyekiti wa bodi na suala la bodi ni la waziri," alisema

CAG kuchunguza TPB

Kwa upande wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), kamati hiyo imetilia shaka uhalali wa maombi ya kuidhinisha kufutwa kwa deni la sh. bilioni 1.1 kutoka katika orodha ya madeni ya chombo hicho na kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi upya kuhusu uhalali wa ombi hilo.

Pia imeutaka uongozi wa Benki ya Posta kupitia upya mahesabu hayo ambayo imewekwa katika orodha ya kufutwa kwa kuwa wana shaka kama kweli hayakusanyiki yote au kuna ujanja kwa baadhi ya watendaji.

Bw. Kabwe aliutaka uongozi huo kuwasilisha takwimu za wadaiwa kuanzia milioni 50 ambao walitakiwa kufutiwa mikopo yao ili wajiridhishe kama hawana uwezo wa kulipa au la.

Bw. Kabwe alisema kutokana na uzoefu alionao mashirika hurundika madai makubwa ya watu walioshindwa kulipa, lakini sh. bilioni 1.1 ni fedha nyingi, jambo ambalo haliwezekani kufutwa kwa urahisi bila kufanya uchunguzi wa kina.

"Maduhuli yaliyoko katika mashirika ya umma ni makubwa ambapo ubadhilifu unafanywa na watu wakubwa," alisema Bw. Kabwe.

Alisema haiwezekani mikopo ya thamani hiyo ifutwe kwa madai ya mkopaji kukosa uwezo wa kurejesha na kuweka wazi kuwa kuna mbinu nyingi za ujanja ambazo hutumiwa na wakubwa za udanganyifu wa taarifa za mali ili kufanya ufisadi na kujipatia mamilioni ya fedha za walipa kodi.

"Tulipowauliza shirika la nyumba thamani ya mali zao walisema sh. milioni 300 lakini tulipofanya ukaguzi tulikuta thamani ya mali za milioni 800," alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo ikifika kipindi cha kuuza mali wanauza kwa sh. mil. 300 na wao kujipatia milioni. 500 kutokana na jasho la Watanzania masikini, jambo ambalo wao hawalikubali ni lazima wapate takwimu sahihi kabla ya kuendelea na hatua nyingine.

Mrema kutinga kwa Pinda, JK

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC),  Bw. Augustino Mrema alisema ana mpango wa kukutana na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)m, Bw. George Mkuchika, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete kuangalia jinsi ya kumaliza uozo wa wizi wa fedha za umma unaodidimiza maendeleo ya nchi.

Alisema nchi iko hatarini kusambaratika kutokana na kukithiri kwa wizi wa fedha za umma unaofanywa na baadhi ya watumishi wa halmashauri za wilaya nchini na kwamba hamati yake haiwezi kuvumilia hali hiyo.

Bw. Mrema alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara katika halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, ambayo alisema inakusanya sh. milioni 200 kati ya sh. bilioni 2.2 ambazo wanatakiwa kukusanya katika mwaka 2011/2012.

"Kuna sh. milioni 766 nyaraka zake hazionekani, cha ajabu mweka hazina amehamishwa, hivi kweli serikali yetu ipo makini?" alihoji Bw. Mrema na kuongeza.

Alisema mwaka 2009 zaidi ya sh. milioni 700 za mapato hazikukusanywa huku mwaka 2010 sh. milioni 838 nazo zilibaki bila kukusanywa katika kiwanda cha miwa, jambo linalozuia wasiwasi ya kuwepo kwa wizi wa fedha hizo baada ya baadhi ya watumishi kuhusika kwa njia moja au nyingine.

Imeandaliwa na Salim Nyomolelo na Flora Amon

4 comments:

  1. WABUNGE MJUE KUWA HALI YA WIZI WA FEDHA ZA UMMA UMEFIKIA HATUA HIYO KUTOKANA NA WATUMISHI KUONA WEZI WANALINDWA NA KUPANDISHWA VYEO.

    ReplyDelete
  2. Mmesema Wilaya zote nchini kwa ujumla wake, lakini hali ni ngumu kule Geita, nilikuwepo juzi kwa jamaa yangu mwl, anasema mwl anaeiba sana na kuwagaia wakubwa hupandishwa cheo ndani ya muda mfupi sawa na walimu wa kike wanaojilegeza kwa wakuawa, twafwa.

    ReplyDelete
  3. KAMA WATU WAMESHINDWA KULIPA DENI LA BENKI YA POSTA WANATAKIWA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KUJIBU MASHTAKA NA WALA SI KUFUTIWA DENI...INA MAANA NANI ANAPASWA KULIPA DENI? TUWE WAKWELI NA WASTAARABU WA KARNE YA 22. WAHUSIKA WALIPE DENI NA KAMA WAMESHINDWA WACHUKULIWE MALI ZAO. BENKI INAFANYA BIASHARA SI KUTOA FEDHA ZA WAVUJA JASHO KWA WATU WACHACHE.

    ReplyDelete
  4. Ukweli ni kwamba tangia RICHMOND kila mtumishi ameona kinachofanyika kutoka juu!Kama JK angetoka asubuhi yake na kutanganza vita dhidi ya UFISADI na kuwataja nani hawa Richmond Kuwasweka RUMANDE na kuchukua mkondo wa sheria ,Waqtumishi wote wangeheshimu taratibu zilizopo, Kama nchi ni aibu kubwa,USALAMA WA TAIFA <POLISI wote hawa Wameshindwa kufanya tathinimini ya kilicho isibu nchi yetu na wizi wa kila siku.
    nachelea kusema kuwa dhambi hii itamwandama JK mpaka kaburini ,kwa kushindwa kusema ukweli wa wizi kwa nchi.Ni kama kukaakimya alitoa ruhusa kwa wezi kuchukua chao mapema. Sasa Mrema na Zitto wanapojitahidi kutafuta ukweli watagundua madhambi mengi sana ambayo JK alikuwa na nafasi kuyazuia , Tabia ya kulindana inadidimiza nchi na sisi tunabaki masikini na wenzetu wachache waliopo kwenye system wamekuwa mabilionea CCM oyee!HAMTAZIKWA NA UTAJIRI ,MUTAVIACHA TU.ISHI KAMA MFALME KUFA KAMA SHETANI.

    ReplyDelete