06 October 2011

TFF kuzishitaki Vancouver, DT Long

Na Zahoro Mlanzi

SIKU moja baada ya timu za Vancouver Whitecaps ya Canada na DT Long ya Vietnam kuwazuia wachezaji, Nizar Khalfan na Danny Mrwanda kuja nchini, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), limepanga kuzishtaki timu hizo kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga mara baada ya waandishi wa habari kutaka maelezo ya kina juu kuhusu ujio wa wachezaji hao, ambao mara kadhaa wamekuwa wakizuiliwa na timu zao, pindi wanapohitajika kuitumia timu ya taifa 'Taifa Stars.

Akizungumzia suala hilo Tenga, alisema hawawezi kuendelea kulichekea kitu hicho na watalazimika andikia barua FIFA kuwaeleza hali hiyo kwa kuwa si mara ya kwanza na inaonekana ni dharau.

Awali Katibu Mkuu wa TFF Angetile Osiah, alieleza kwamba Septemba 15, mwaka huu waliiandikia barua Vancouver kuwaeleza kumhitaji Nizar kujiunga na timu yake ya taifa, lakini uongozi wa timu hiyo ukawajibu kwamba hawajaipata barua hiyo.

"Nilipokwenda kuangalia siku tuliyotuma tuliona ni Septemba 15, tulishangaa iweje wadai hawajaipata huku wakisema waliipata ile ya awali, ambayo tulimuombea kwa ajili ya mchezo dhidi ya Algeria na hata tulipomuuliza Anderson (Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo), ambaye ndiyo tunafanya naye mawasiliano mara kwa mara naye alidai hakuipata," alisema Osiah.

Alisema baada ya mkanganyiko huo, waliamua kutuma nyingine ambapo ndipo walipoambiwa muda umepita na hawataweza kumruhusu kuja kujiunga na Taifa Stars.

Akizungumzia suala la Mrwanda, alisema kwa kawaida hutuma tiketi mbili katika mtandao wa Mrwanda baada ya wa Abdi Kassim 'Babi' ambaye wanacheza timu moja kutoupata, lakini wanashangaa Babi amekuja Mrwanda hajafika.

Lakini walipomuuliza Babi kuhusu Mrwanda, alisema amebaki Vietnam baada ya Mwenyekiti wao kumhitaji abaki kuzungumzia masuala ya mkataba mpya na timu hiyo.

No comments:

Post a Comment