06 October 2011

Miaka 50 ya Uhuru TFDA yapata mafanikio

Na Heri Shaaban

MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imepata  mafanikio katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika udhibiti
wa ubora wa bidhaa.

Hayo yalisemwa na Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Hiiti B. Sillo wakati alipozungumza na  waandishi wa habari.

Bw. Sillo alisema kuwa mafanikio hayo yamepatikana baada mamlaka kuimarisha mifumo ya kutathimini na kusajili vyakula, dawa vipodozi na vifaa tiba.

"Katika kipindi hicho TFDA shughuli za udhibiti wa bidhaa hususan vyakula na dawa zilianza enzi za ukoloni kutokana na mabadiliko ya kisayansi na teknolojia, kiuchumi na kijamii kumekuwepo na mabadiliko ya mifumo ya udhibiti wa bidhaa," alisema Bw. Sillo.


Alisema kuwa ili kuhakikisha usalama na ubora wake kabla  vyakula na dawa havijauzwa katika Soko la Tanzania, katika miongo minne ya awali utaratibu huu ulikuwa haufanyiki isipokuwa kulikuwa na njia mbadala ya kuhakikisha usalama ya bidhaa kabla kutumiwa.

Bw. Sillo alisema kuwa usajili wa dawa ulianza 1992 wakati wa upande wa vyakula kulikuwa na utaratibu wa upimaji vyakula kabla kupewa kibari cha biashara.


Alisema TFDA ilipoundwa 2003 ilijenga mifumo ya usajili wa bidhaa ambayo inahusisha tathimini na nyaraka zenye taarifa za kitaalam za bidhaa, uchunguzi wa kimaabara na sampuli za bidhaa na ukaguzi wa viwanda vya ndani na nje ya nchi.

"Ilipofika Juni 2011 jumla ya dawa za binadamu 3,688 na dawa za mifugo 472,vipodozi 1,222 na vifaa tiba 11 vilikuwa vimesajiliwa na TFDA,aidha vyakula vilivyofungashwa 2,351 vilisajiliwa tangu kuanza kwa utaratibu huu," alisema.

Pia alisema kuwa mfumo wa ukaguzi na ufuatiliaji wa vyakula na dawa ulianza kutekelezwa baada sheria ya 1978 kutungwa na kanuni mbalimbali za vyakula ikiwa ni pamoja na ile ya udhibiti wa uingizaji wa vyakula kutoka nje ya nchi zilizotungwa 1980.

No comments:

Post a Comment