06 October 2011

Julio aahidi makubwa Coastal

Na Mashaka Mhando, Tanga

KOCHA mpya Coastal Union ya jijini hapa Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’, ameahidi ushindi kwenye mchezo wake dhidi ya Villa Squad, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani
Jumamosi.

Akizungumza jijini hapa juzi, mara baada ya kumaliza mazoezi na kikosi hicho, Julio alisema wachezaji aliowakuta watampa ushindi wa kwanza Jumamosi na akawataka wapenzi, mashabiki na viongozi wa timu hiyo kumpa ushirikiano, ili aweze kutimiza malengo yake ya kuibakiza timu hiyo katika Ligi Kuu msimu ujao.

Alisema kikosi chake, si kibaya kwani alipata muda wa kukisoma katika mchezo dhidi ya Yanga ambapo timu hiyo ilikung’utwa mabao 5-0, isipokuwa tatizo aliloligundua ni wachezaji wengi kukosa ‘stamina’ na uwezo wa kukabiliana na wapinzani wao.

“Siwezi kumlaumu kocha aliyepita, lakini timu nimeiona ina upungufu mwingi hasa wa kukosa nguvu, ingawa kila mchezaji amekuwa na uwezo binafsi, ambao nitaufanyia kazi kipindi hiki ili kuhakikisha tunafanikiwa. Dhamira yangu ni kuibakisha Ligi Kuu timu hii.

“Naomba ushirikiano kutoka kwa viongozi, wapenzi na wanachama wa klabu hii na hawa wachezaji wakifuata maelekezo ninayotaka, naamini malengo yetu yatafanikiwa na kwa kuanza, mchezo unaofuata tutashinda tu,” alisema.

Katika mazoezi yaliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Gymkhana jijini hapa, kocha huyo alionekana kuwapa mazoezi mazito ambapo baadhi ya wachezaji walionekana kulalamika maumivu ya tumbo kutokana ugumu wa mazoezi, akiwemo beki Edwin Mukenya.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo Salim Bawazir, alisema Mukenya awali walimsajili lakini walimwondoa kwenye usajili huo baada ya kuhitilafiana, ila sasa watamsajili katika dirisha dogo Januari mwakani.

Julio amechukuliwa na timu hiyo kuinusuru, akichukua mikoba ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Hafidh Badru. Julio ambaye hata hivyo mkataba wake haukuwekwa wazi atasaidiwa na Ali Jangalu.

No comments:

Post a Comment