03 October 2011

Simba Cement yakabidhi msaada wa darasa,samani

Na mwandishi wetu, Urambo

KAMPUNI ya saruji Tanga kupitia bidhaa yake ya Simba imekabidhi vyumba viwili vya madarasa, madawati 40 na matundu mawili ya choo kwa Shule ya Sekondari Kapuya
iliyoko katika Kata ya Kaliua, Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora.

Akikabidhi msaada huo katika hafla iliyofanyika Kaliua mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mauzo Kanda ya Kati wa kampuni ya Tanga Cement, Bw. Deogratias Mutalemwa, alisema msaada huo umewezekana kwa kupitia mpango wa kampuni hiyo kuisaidia jamii (CSI)

Alisema kupitia mpango huo kampuni ya Tanga Cement imekuwa ikitilia mkazo maeneo makuu manne ambayo ni afya, maendeleo ya jamii, mazingira na elimu.

“Napenda kuwakumbusha kupitia mpango huu na bidhaa yetu ya simba tunakabidhi majengo haya na samani zake vikiwa na thamani ya sh. milioni 48.5 tukiamini kuwa elimu bora hutolewa darasani hivyo kitendo hiki ni mwanzo mzuri katika suala la upatikanaji elimu bora japo majengo na samani peke yake havitoshi,” alisema.

Ni kutokana na hilo mkuu huyo wa mauzo aliomba marafiki na wafadhili wengine kuungana na  Tanga Cement kusaidia juhudi za serikali ya Tanzania katika mipango yake katika kuendeleza elimu nchini.

Awali akisoma risala ya shule katika hafla hiyo Mkuu wa Sekondari,Bw. Benny Walter, alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mabweni ya kulala wanafunzi, jambo linalofanya wanafunzi wengi kukaa mbali na shule na hata wale wanaoishi maeneo jirani wanaishi katika maeneo ambayo si rafiki wa elimu.

Mkuu huyo alizitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa walimu,  vyumba vya madarasa, vitabu vya kufundishia na nyumba za walimu kuwa baadhi ya matatizo yanayoikabili shule hiyo iliyoanza Januari 2011 ikiwa na wanafunzi 80 na hadi sasa idadi ikifikia 130 baada ya wengine kuhamia.

“Ni kutokana na changamoto hizi pamoja na kuishukuru kampuni ya Tanga Cement kwa msaada huu tungewaomba waendelee kutushika mkono pamoja na wengine wenye mapenzi mema na elimu ya watoto wetu  ili tuweze kuzishinda changamoto hizi”, alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Kaliua,Bw. Nestory Hoka, aliyepokea madarasa hayo kwa niaba ya mbunge wa Urambo Mashariki, Prof Juma Kapuya alisema kitendo kilichofanywa na kampuni hiyo kinapaswa kuigwa, kwani kinaonesha ni jinsi gani Tanga Cement inavyojali maendeleo ya elimu katika nchi ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment