05 October 2011

Nchimbi awatolea uvivu viongozi wa michezo

Na Addolph Bruno

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Emmanuel Nchimbi, amesema hali ya michezo iliyopo sasa nchini ni mbaya na sababu iliyosababisha ni viongozi
kulipaka rangi jambo hilo.

Waziri Nchimbi, alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizindua Baraza jipya la Michezo la Taifa (BMT), aliloliteua wiki iliyopita.

Katika uzinduzi huo, Nchimbi aliwataka viongozi aliowateua kuanza majukumu yao, huku wakitambua kuwa hakuna mchezo hata mmoja unaoridhisha hadi sasa.

"Jambo la msingi ambalo mnapaswa kulitambua ni kwamba hali ya michezo ipo nyuma sana na kosa ambalo tunalifanya na limetufikisha hapa tulipo ni kulipaka rangi jambo hili, mimi binafsi nina imani hamtatuangusha.

"Kwa mfano katika mashindano ya All Africa Games (Mashindano ya Afrika), zaidi ya michezo kumi inashiriki, sisi tulipeleka michezo sita tena wachezaji wake walifanya maandalizi ndani ya mwaka huu, hapa tanaweza kupima na kuona kazi kubwa inayotukabili," alisema Nchimbi.

Aliwashauri viongozi hao wa BMT chini ya Mwenyekiti mpya Deoniz Malinzi, kuandaa mpango na mfumo mpya wa utendaji wa kazi ambao utasaidia hata kuishawishi Serikali, kuiongezea bajeti wizara hiyo ambayo kwa sasa pato lake ni dogo, ikilinganishwa na baadhi ya wizara zingine.

"Uandaliwe mpango maalumu, kila chama kieleze mpango wake na baada ya kuipata mipango ya vyama vyote, hiyo sasa isaidie kutengeneza mpango wa baraza ambao utakuwa mwongozo," alisisitiza Waziri Nchimbi.

Waziri huyo aliwaagiza wajumbe na viongozi wa baraza hilo, kushirikiana kikamilifu na vyama vya michezo katika kazi zao za kila siku, ili kujenga mahusiano yenye tija na kuimarisha hali ya michezo nchini.

Nchimbi alisema kufanya kazi kwa kutambua mfumo wa taasisi za kuibua vipaji na kuzingatia ushirikiano na majeshi ya ulinzi na usalama kutokana na jitihada zao nzuri, huku akitolea mfano Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Naye Malinzi, alimshukuru Waziri Nchimbi kwa kuteua baraza hilo na kumhakikishia kuwa limeanza kufanya kazi yake rasmi, mara baada ya uzinduzi huo mapema jana.

Alisema amesikitishwa kuona Tanzania, ambayo ina zaidi ya watu milioni 40 haina mchezo hata mmoja, ambao unafanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, jambo ambalo watalifanyia kazi.

No comments:

Post a Comment