Na Addolph Bruno
TIMU zilizonyakua ubingwa katika mchezo wa kikapu katika nchi za Afrika Mashariki na kati, zinatarajiwa kuanza kuwasili kuanzia Oktoba 7 mpaka 8, mwaka huu kwa
ajili ya mashindano ya Klabu Bingwa kwa nchi hizo yatakayofanyika nchini.
Mashindano hayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi Oktoba 9 hadi 16, mwaka huu katika Uwanja wa ndani wa Taifa na Uwanja wa Don Bosco Upanga, Dar es Salaam ambavyo vimeteuliwa kwa ajili ya mtanange huo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Alexander Msofe alisema maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri.
"Kila kitu kinakwenda vizuri kwa ujumla, hayo ninayoyasema ni pamoja na maandalizi mazuri ya viwanja, Uwanja wetu wa ndani wa Taifa na ule wa Don Bosco, Upanga vipo katika uangalizi mzuri kwa kifupi kila kitu kipo sawa," alisema Msofe.
Alisema timu kutoka nchi za Uganda na Kenya, zimethibitisha kutua nchini Oktoba 7 huku Ethipia na timu nyingine zinatarajiwa kutua Oktoba 8, mwaka huu.
Msimu uliopita mashindano hayo yalifanyika Burundi ambapo timu ya Kenya Port Authority (KPA), ilitwaa ubingwa.
No comments:
Post a Comment