06 October 2011

Mgawo wa umeme wafunga kiwanda

Na Grace Michael

NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga ameshuhudia madhara ya mgawo wa umeme baada ya kukuta kiwanda cha uzalishaji mifuko ya plastiki kimefungwa na
wafanyakazi wake kusimamishwa kazi.

Dkt. Mahanga alikutana na hali hiyo jana katika kiwanda cha Tropical Plastics kilichopo Chang’ombe, Dar es Salaam ambapo alielezwa kuwa uongozi wa kiwanda hicho umeamua kusimamisha uzalishaji kutokana na kukosa umeme wa uhakika.

Akielezea hali hiyo Ofisa Usalama wa kiwanda hicho, Bw. Yusuph Mape alisema kuwa kiwanda hicho kilikuwa na zaidi ya wafanyakazi 30 ambao kwa sasa wamesimamishwa kazi hadi makali ya mgawo yatakapopatiwa ufumbuzi.

“Tunapoona umeme upo huwa tunawaita wafanyakazi kama sita hivi na ndio maana hapa hata Mkurugenzi mwenyewe hayupo, nipo tu mimi na walinzi wenzangu,” alisema Bw. Mape.

Baada ya kukutana na mazingira hayo, Dkt. Mahanga alisitisha ukaguzi kiwandani hapo na kutoa maagizo kwa uongozi wa juu kuwasilisha ripoti ya namna kinavyofanya uzalishaji, idadi halisi ya wafanyakazi na kinavyozingatia usalama wa mahala pa kazi.

“Tumefika hapa kwa lengo la kuona namna wafanyakazi wanavyofanya kazi, mazingira waliyonayo ili tusikilize matatizo yanayowakabili, lakini bila kuwepo wafanyakazi hatuwezi kufanya chochote, hivyo namwagiza mkurugenzi kuwasilisha kwangu ripoti kabla ya Jumatano wiki ijayo,” alisema Dkt. Mahanga.

Kilio hicho cha umeme pia kiliibuka katika kiwanda cha nguo cha Namera kilichopo Gongolamboto, Dar es Salaam, ambapo wafanyakazi walieleza kuwa mgawo huo unawaathiri hata wao kwa kuwa wanashindwa kutimiza malengo waliyojiwekeza ya uzalishaji.

Akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho, Dkt. Mahanga aliambiwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni mgawo wa umeme, hivyo waliiomba serikali kuangalia uwezakano wa kutoa kipaumbele zaidi katika viwanda ili kuzalisha zaidi.

“Muda mwingi tunautumia kukaa tu bila kazi, hivyo hata wawekezaji nao watafika wakati watashindwa hata kutulipa inavyotakiwa na vipato vyetu vitaathirika kwa kiasi kikubwa,” alisema Bw. Christopher William ambaye ni mfanyakazi wa kiwandani hapo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Namera, Bw. Hasnain Pardesi, alisema kuwa matatizo makubwa yanayowakabili kama kiwanda ni ukosefu wa umeme wa uhakika na ukosefu wa wahandishi katika sekta ya nguo, hivyo kulazimika kuleta wataalamu kutoka nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, wafanyakazi hao waliiomba serikali kuharakisha mchakato wa kuangalia kima cha chini cha mshahara kwa kuwa kilichopo sasa hakikidhi mahitaji halisi ya maisha.

Akijibu oambi hilo, Dkt. Mahanga aliwataka kuvuta subira wakati suala hilo likifanyiwa kazi kwa kuwa tayari bodi za mishahara kisekta zipo na zinatarajiwa kutoa mapendekezo ambayo yanaweza kuwaridhisha wafanyakazi wa sekta binafsi.

Alisisitiza umuhimu wa wafanyakazi hao kuanzisha chama cha wafanyakazi ambacho kinaweza kusaidia kuondoa migogoro isiyo na tija mahala pa kazi.

“Hakikisheni wafanyakazi hawa wanaanzisha chama cha wafanyakazi, lakini pia menejimenti na nyie mnatakiwa kuhakikisha mna mahusiano mazuri na wafanyakazi wenu, hawa ndio njia pekee ya kuongeza uzalishaji kwa kuwa watafanya kazi kwa kujituma,” alisema Dkt. Mahanga.

Kiwanda cha Namera kina jumla ya wafanyakazi 400, ambapo uongozi wake umeahidi kutoa ushirikiano wa wafanyakazi ili wawe na chama chao.

No comments:

Post a Comment