Na Amina Athumani
MENEJA wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu kwa Wanawake wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Maryline Tana, amesema
kongamano la soka la wanawake litakaloendeshwa leo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), litakuwa ni mfumo bora kwa soka la wanawake barani Afrika.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Maryline alisema ni mara ya kwanza kwa Afrika kuandaliwa kwa kongamano kama hilo, ambalo litatoa mikakati ya masoko na udhamini katika soka la wanawake Tanzania na Afrika.
Alisema kongamano hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuunga mkono soka la Tanzania na kwamba, itakuwa ni ufunguo kwa nchi za ukanda wa Afrika kuandaa makongamano kama hayo.
Kongamano hilo litashirikisha wadau 130 wa soka nchini, ambapo mada kubwa ni maendeleo ya soka la wanawake.
"Kongamano hili litatafuta na kupokea maoni ya wadau mbalimbali katika kuhakikisha soka la wanawake linapiga hatua na kutafuta njia ya kupata wadhamini," alisema Maryline.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA), Lina Mhando, alisema inawezekana idadi hiyo ya washiriki ikawa ni ndogo, lakini wamewataka wadau kulifahamu hilo kwani wasingeweza kuwaita watu wote kwa ajili ya kushiriki.
Alisema kongamano hilo litakuwa la siku tatu ,ambapo kutakuwa na tamasha maalum litakalofanyika katika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, litakaloshirikisha timu mbalimbali za wanawake.
Alisema kutakuwepo na timu za wachezaji wenye miaka chini ya 14 kutoka katika shule mbalimbali na mechi za viongozi wanawake, waandishi wa habari na waalimu wa shule za msingi.
No comments:
Post a Comment