Na Zahoro Mlanzi
BEKI wa timu ya taifa 'Taifa Stars' na Simba, Amir Maftah leo anatarajia kupata majibu ya mwisho kuhusu hatima yake ya kifundo cha mguu kama atafanyiwa upasuaji au
kuwekwa plasta gumu (POP), baada ya kufanyiwa vipimo.
Beki huyo wa kushoto, aliumia wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, ambapo timu hizo zilitoka suluhu.
Akizungumza kwa simu Dar es Salaam jana, Maftah alisema maumivu ya kifundo cha mguu yanamtesa kwani yanamuuma ndani kwa ndani, kitendo ambacho kinampa wakati mgumu kufanya mambo yake.
"We acha kaka! mguu unanitesa mbaya, jana nimeanza mazoezi ya gym kuweka mwili sawa lakini bado nasikia maumivu ya ndani katika kifundo cha mguu, hivyo nikiamka salama kesho (leo) nitakwenda hospitali ya IRR, kumuona daktari kwa uchunguzi zaidi," alisema Maftah.
Alisema kwa jinsi maumivu anavyoyasikia, anahisi anaweza kufanyiwa upasuaji au kuwekwa POP ndipo tatizo alilonalo linaweza kumalizika na kurudi katika hali yake ya kawaida.
Pamoja na kuumia, lakini Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen alimwita katika kikosi chake kitakachocheza na Morocco Oktoba 9, mwaka huu katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwakani (CAN 2012).
Lakini siku mbili baada ya kutangaza kikosi chake na kupata taarifa kwamba beki huyo anatakiwa awe nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki mbili, ndipo alipoenguliwa na nafasi yake kuchukuliwa na beki mwenzake wa Simba, Juma Jabu.
Simba kwa sasa inajiandaa na mchezo wao wa Oktoba 16, mwaka huu dhidi ya African Lyon katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Timu hiyo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 18 ikifuatiwa na JKT Oljoro yenye pointi 16.
No comments:
Post a Comment