*Kukaa nje wiki nne
Na Frank Balile
NAHODHA wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa ameumia nyonga kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa
Karume, Dar es Salaam.
Katika taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kwa mujibu wa daktari wa Taifa Stars, Dkt. Mwanandi Mwankemwa, maumivu hayo yatamweka Nsajigwa ambaye pia ni nahodha wa Yanga nje ya uwanja kwa kati ya wiki mbili hadi nne.
Wambura alisema kutokana na ushauri wa daktari, Kocha Jan Poulsen amemuondoa kwenye kikosi hicho ambacho kitasafiri Oktoba 6 mwaka huu kwenda Casablanca, Morocco kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Oktoba 9.
Mechi hiyo ni kuwania kufuzu michuano ya Afrika itakayofanyika mwakani katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.
Alisema badala yake Kocha Poulsen amemwita kwenye timu yake Nassoro Masoud Said ‘Cholo’ wa Simba kuziba nafasi ya beki huyo wa pembeni.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema wachezaji wanaocheza nje ya nchi walioitwa na Kocha Poulsen, wameanza kuwasili.
Alisema Idrissa Rajab anayechezea Sofapaka ya Kenya na Mbwana Samata wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wamewasili jana jioni na tayari wameripoti katika kambi ya Taifa Stars.
Wambura alisema Henry Joseph wa Kongsvinger IL ya Norway), Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada) na Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden) walitarajiwa kuwasili jana usiku kwa ndege ya KLM.
Alisema washambuliaji Abdi Kassim na Dan Mrwanda, wanaochezea timu ya DT Long An ya Vietnam ndiyo watakaokuwa wa mwisho kujiunga na kambi ya Stars, ambapo watawasili nchini leo saa 7 mchana kwa ndege ya Qatar Airways.
No comments:
Post a Comment