06 October 2011

Ferguson: Rooney kuvunja rekodi ya Charlton

LONDON, England

KOCHA wa Manchester United Sir Alex Ferguson, anaamini kwamba mchezaji Wayne Rooney, atavunja rekodi ya Sir Bobby Charlton ya kufunga mabao na kumfanya muda
wote awe mfungaji bora wa klabu hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Hbarai la Marekani (AP), kocha huyo alisema hivi sasa mchezaji huyo ana umri wa miaka 25, jambo ambalo linamfanya kuwa na miaka mingine mitano ya kuendelea kuwa mfungaji bora.

"Kwa sasa ana miaka 25, hivyo unaweza kudhania bado ana miaka mingine mitano kuwa katika kiwango cha juu," aliiambia tovuti ya klabu hiyo.

"Unapomwangalia ni kama Ryan Giggs, anaweza kucheza vizuri katika umri wa miaka 30, hivyo fursa ipo na muda upo upande wake," alisema.

Hadi sasa Rooney ameshawafungia mabao 156 mashetani hao wekundu, idadi ambayo bado yupo nyuma kwa mabao 100 kumfikia Charlton, ambaye aliweka rekodi ya mabao  249, lakini Sir Alex anadhani mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 anaweza kuvunja rekodi hiyo kuanzia msimu huu.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya England, ameuanza msimu huu kwa kiwango cha hali ya juu akiwa ameshafunga mabao tisa yakiwemo matatu matatu aliyoyapachika kwenye mechi dhidi ya Arsenal na  Bolton Wanderers.

No comments:

Post a Comment