24 October 2011

Hoja binafsi ya sheria ya albino kuwasilishwa

Na Faida Muyomba, Geita

MBUNGE Jimbo la Lindi, Bw. Salum Barwani (CUF), ameahidi kupeleka hoja binafsi bungeni wakati wa kikao kijacho, akitaka
kuwepo sheria itakayokomesha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(albino) nchini.

Pia wanasiasa nao wametakiwa kuanzisha kampeni maalumu kupinga ukatili dhidi ya walemavu hao, badala ya kuandamana nchini kwa lengo la kupinga ufisadi peke yake.

Hayo yalisemwa na mbunge huyo ambaye pia ni albino,wakati yeye na viongozi wenzake kutoka Chama cha Albino Tanzania (TAS),  walipokuwa wilayani Geita juzi, kumjulia hali mtoto aliyenusurika kuuawa kwa
kukatwa vidole vyake.

"Hili ni jambo la hatari kabisa kwetu, kwani hawa watu wamekusudia kutuangamiza...ili kuonesha kwamba hii ni vita nimejiandaa
kupeleka hoja binafsi kwa spika juu ya ukatili huu wakati wa kikao kijacho cha
Novemba.’’Alisema
mbunge huyo kwa msisitizo mkubwa.

Alisema ukatili pamoja na mauaji dhidi ya watu hao yamekuwa yakikithiri kila siku hapa nchini, kutokana na kutokuwepo sheria inayowalinda, hali inayosababisha 'wafanyabiashara' ya viungo vya albino kuendelea kutamba kila kona ya
nchi.

Alisema watu hao wamefanya albino kuishi maisha ya hofu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAS,Bw.Ernest N. Kimaya, alitaka kuwepo kwa kura maalumu za maoni kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya kuwatambua wauaji na wanunuzi viungo vya albino ili kukomesha tatizo hilo.

"Kura za maoni kwa watu wanaoua albino pekee kwa kanda ya ziwa, zipigwe tena kubaini mzizi wa tatizo hili. Hatutaki sisi albino tuondoke katika jamii ya watu wa Tanzania, tunataka tuendelee kuwepo na tuishi kama watu
wengine.’’Alisisitiza.

Akiwa hospitali ya wilaya ya Geita,alikolazwa mtoto, Adam Robert(14),Mwenyekiti huyo alipiga marufuku watu wasio fahamika kuingia na kupiga picha za mtoto huyo kwa kile alichosema  wengi wao wanalengo kufanyia biashara hasa nje ya nchi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Albino Mkoa wa Mwanza, Bw.Alfred Kapole, alitaka wanasiasa waanze kuonesha mchango wao kwa albino kwa kuelimisha wafuasi wao majukwaani ili kuonesha uthamini kwa walemavu hao, kwani nao ni wapiga kura muhimu.

No comments:

Post a Comment