Na Esther Macha, Mbeya
DEREVA wa Lori aina ya fuso iliyosababisha vifo vya watu 14 Wilayani Chunya mkoani hapa Septemba 24 mwaka huu Bw. Moses Kapus (55)amesomewa mashitaka 44 chini ya
ulinzi wodini Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Msangamwelu
saa 1: 00 usiku baada ya lori hilo namba T 582 AJF kupinduka likitokea mnadani Mbuyuni wilayani Chunya kufuatia kushindwa kupanda mlima na kuanguka.
Akimsomea mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya hakimu mkazi wa Wilaya Bw.Michael Mteite, Wakili wa Serikali Bw.Griffin Mwakapeje, alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na makosa 44.
Katika mashitaka hayo Bw.Mwakapeje alidai kuwa mshtakiwa bw. Kapus akiwa kama dereva alisababisha ajali kwa uzembe kutokana na kuendesha kwa kasi na kusababisha vifo vya watu 14.
Wakili huyo alidai kuwa dereva huyo akiwa na gari aina ya fuso namba T582 AJF aliendesha gari hilo kwa mwendo wa kasi na kusababisha majeruhi 43 ambao mpaka sasa hali zao hazijatengamaa.
Alidai mshitaki huyo alisababisha ajali hiyo baada ya kutumia gari hilo kinyume na masharti aliyopewa.
Kwa upande wake Hakimu wa Mahakama hiyo Bw.Mteite alisema mahakama imepokea
makosa yote alisomewa mshitakiwa 44.
Hata hivyo mshitakiwa aliomba mahakama impe dhamana kutokana na hali yake kuwa mbaya kiafya.
Hata hivyo wakili wa serikali alimwomba Hakimu huyo kuangalia masharti ya dhamana kwanza na yawe magumu kutokana na hali za majeruhi kuwa mbaya.
Hakimu Mteite alimtaka mshitakiwa kuwa na fedha taslimu sh. milioni tano na wadhamini wawili wenye nyumba ili aweze kupata dhamana.
Hata hivyo wakili wa serikali alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kesi hiyo kutajwa tena Octobar 17 mwaka huu.Hata hivyo mtuhumiwa huyo alikosa dhamana kutokana na kushindwa masharti.
No comments:
Post a Comment