04 October 2011

CHADEMA wadaiwa kumpiga diwani CCM,kuchoma gari lake

*Ni baada ya kushindwa uchaguzi Moshi

Heckton Chuwa na Martha Fataeli,Moshi

DIWANI wa Kata ya Uru Kaskazini Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro Bw. Evarist Momburi, (53), amepigwa na kujeruhiwa huku gari lake
likichomwa moto na kuteketea kabisa na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Akidhibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Absalom Mwakyoma, alisema lilitokea Jumapili katika kijiji cha Uru Mrawi.

Alisema tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya matokeo ya uchaguzi mdogo wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho uliofanyika siku hiyo kutangazwa ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliibuka mshindi.

“Uchaguzi uliandaliwa baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho kukihama chama cha CHADEMA na kurudi Chama Cha Mapinduzi, (CCM).

Muda mfupi tu baada ya msimamizi wa uchaguzi huo Rolanda Tenga, kutangaza matokeo hayo watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CHADEMA walianza vurugu,” alisema.

Alisema katika vurugu hizo watu hao walilipindua gari la diwani huyo kabla ya kulichoma moto na kuungua kabisa gari hilo aina ya Toyota Hilux namba T 171 AFX.

Alisema mshindi katika uchaguzi huo Bw. Roti Mauki, (37) alipata jeraha kwenye jicho lake la kushoto baada ya kushambuliwa na watu hao kwa mawe.

Kamanda Mwakyoma alisema tayari polisi imewatia nguvuni watu saba kati ya hao waliofanya vurugu na kuwataja kuwa ni Evarist Lyamuya, (37), Evokati Venance Nyaki, (35) na Thomas Laurent Sangawe, (23).

Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Evin  Marko, (25); Jonathan Kisima, (32); Tea Kisima, (41) na Rudovic Momboi, (49).

“Bado jeshi la polisi linawatafuta watu wengine wanane kuhusiana na vurugu hizo, ombi letu ni kuwa wajitokeze maana tayari majina yao tunayo,” alisema.

Alitoa wito kwa viongozi na wafuasi wa vyama mbali mbali vya siasa kuzingatia maadili ya uchaguzi pamoja na sheria za nchi ili kuepuka vurugu.

Katika uchaguzi huo Jumla ya watu 437 walipiga kura ambapo mgombea wa CCM Bw. Mauki alipata kura 230 dhidi ya kura 207 za Bw.Kisima wa CHADEMA.

Tukio hilo limetokea siku chache tu baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuhutubia taifa na kuwaonya wanasiasa kuacha vurugu ili kulinda amani ya nchi.

No comments:

Post a Comment