04 October 2011

MAGENDO YA SUKARI

*Kampuni tatu zafutiwa leseni

Heckton Chuwa na Martha Fataeli, Moshi

SERIKALI imezifutia leseni kampuni tatu Aa kusambaza sukari Mkoani Kilimanjaro kwa kushindwa
kutimiza masharti iliyoweka ikishirikiana na wadau mwezi uliopita.

Akitangaza uamuzi huo jana, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe alitaja kampuni hizo kuwa ni Staways Investment, Merenga Investment na Mohamed Enterprises na kwamba uamuzi huo umeanza mara moja.

“Nimemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari nchini awaarifu kwa maandishi wahusika wote kuhusiana na maamuzi haya ya serikali kabla ya saa 6:00 mchana leo (jana),” alisema Prof. Maghembe.

Alitaja moja ya sharti kubwa waliyovunja wazambaji hao kuwa ni pamoja na kuvusha sukari kwenda nchi jirani huku Watanzania wakikosa bidhaa hiyo muhimu.

Alisema serikali imeteua wasambazaji wengine wapya wawili kuanzia jana ambao aliwataja kuwa ni Modern Holdings, (EAC) Limited na KNCU Limited.

Waziri Maghembe alisema serikali imeziagiza ofisi za makatibu tawala wa mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Manyara kuteua wasambazaji waaminifu ili wapewe leseni za kusambaza sukari kwenye mikoa yao.

Aliongeza kuwa serikali imepiga marufuku usafirishaji wa sukari usiku kuanzia saa 12 jioni hadi saa 12 alfajiri na kwamba magari yatakayovunja amri hiyo yatataifishwa pamoja na sukari itakayokamatwa.

Waziri huyo alisema serikali itaongeza ulinzi maeneo ya mipaka ya mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mwanza, Mara na Kagera ili kuhakikisha agizo la kuzuia usafirishaji sukari nje ya nchi kiholela linatekelezeka.

“Serikali pia itaongeza ulinzi kwenye viwanda vyote vya sukari nchini kwa kuweka askari. Natoa agizo kwa uongozi wa viwanda vyote kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa kila siku juu ya kiasi kinachozalishwa na wale wanaouziwa sukari inayozalishwa,” alisema.

Alisema magari yatakayotumiwa kubeba sukari kutoka viwandani pia lazima namba zake za usajili ziorodheshwe sambamba na majina ya wamiliki wa magari hayo, kiasi cha sukari kitakachochukuliwa kwa ajili ya usambazaji na wilaya inapopelekwa.

Aliagiza taarifa hizo kupelekwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na ofisi ya mkoa kiwanda kilichopo kila siku kabla ya saa 12 jioni na kwamba kiwanda au kampuni itakayokaidi agizo hilo itachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungiwa leseni.

Alisema serikali imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya baadhi ya wasambazaji kukataa kutimiza makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali na wadau wa sukari kilichofanyika Septemba 6, mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine waliagizwa kutouza sukari nje ya nchi.

“Tulipeana wiki moja jambo hili likome na sukari iingie sokoni hapa hapa nchini kwa bei ya kati ya 1,800/- na 1,900/- kwa kilo lakini bei inaendelea kupanda hadi kufikia 3,000/- kwa kilo,” alisema.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mmoja wa wasambaji aliyefungiwa alidai kuwa alikuwa hajapokea taarifa hiyo ya serikali, na kuwa alikuwa ameingia mkataba na Kiwanda cha Sukari cha TPC.

No comments:

Post a Comment