Na Livinus Feruzi, Bukoba
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Alex
Malasusa amesema suala la tatizo la umeme linaloendelea
kuikabili nchi halitakiwi kujadiliwa kwa mtazano wa kisiasa, bali kwa misingi ya kulipatia ufumbuzi wa kudumu ili kuokoa maisha ya Watanzania.
Dkt. Malasusa alisema hayo jana Mjini Bukoba, wakati akizungumza na waandishi
wa habari muda mfupi baada ya kufungua mkutano mkuu, uliowakutanisha maaskofu
wa kanisa hilo Tanzania, viongozi wa vyama vya wamissionari na taasisi zake
kutoka Ujerumani, Sweden, Denmark na Amerika.
Alisema suala la umeme si starehe kwamba mtu apate au asipate hasa kwa kuangaliwa kwa mtazamo wa matumizi ya nyumbani tu, bali ni nyenzo kubwa katika uzalishaji mali wa shughuli za maendeleo.
Askofu Malasusa alisema hospitalini vifaa vingi vinategemea umeme na kuwa nchi ikikosa nishati ya umeme na kushindwa kuzalisha itaendelea kuwa maskini, jambo ambalo ni hatari katika ushindani wa soko la Afrika Mashariki.
“Nafurahi kusikia wadau wengi wanajitokeza na kujadili suala umeme, lakini suala hili lazima liangaliwe kwa mapana makubwa si kwa mtazamo wa kuwasha taa na matumizi ya nyumbani.”
Alisema Watanzania kwa pamoja wanatakiwa kukaa na kutafakari kwa kina jinsi
ya kutatua tatizo hilo la upungufu wa nishati ya umeme nchini kwa maendeleo
ya nchi na Watanzania kwa ujumla.
Kuhusu tuhuma zilizotolewa na serikali juu ya viongozi wa dini kujihusisha
na uuzaji wa dawa ya kulevya, Dkt. Malasusa alisema si wakati wa serikali
na viongozi wa dini kuanza kulumbana, wakati utafika wa kupata ukweli juu ya suala hilo.
Naye Mwenyekiti wa Mkutano huo Askofu Dkt. Stephen Munga, alisema ukosefu wa
umeme nchini umeleta madhara ikiwa ni pamoja na kuharibu uwekezaji.
Alisema ni tatizo nchi kukosa umeme wa uhakika kwa kipindi cha miaka 50 tangu
kupata uhuru, jambo ambalo linatokana na kukosekana kwa utawala bora.
Mkutano huo wa siku tatu unatarajia kujadili masuala mbalimbali ya
kimaendeleo ikiwa ni pamoja na hali ya uhusiano kanisa la KKKT na washirika
wao, miaka 50 ya uhuru wa Tanzania na kiasi gani kanisa linavyoweza kujitegemea au kuendelea kuwa tegemezi.
No comments:
Post a Comment