19 October 2011

Ahadi ya Bajaj kwa wajawazito ngumu-Wabunge

Na Tumaini Makene

MOJA ya ahadi za Rais Jakaya Kikwete alizoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, inayohusu matumizi ya pikipiki aina
ya bajaji kwa ajili ya kuwabeba akina mama wajawazito kwenda kujifungua, imezua mjadala katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ambapo baadhi ya wabunge wamesema haitekelezeki.

Wamesema kuwa serikali inapaswa kujielekeza katika kutatua tatizo la usafiri kwa wagonjwa, hasa akina mama wajawazito maeneo ya vijijini, kwa kutumia magari ya wagonjwa 'ambulances' badala ya bajaj au pikipiki za matairi matatu, huku mwingine akishauri zitumike boti katika baadhi ya maeneo nchini.

Mbali ya hilo, PAC chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. John Cheyo imeiagiza serikali kuanza kufikiria uandikishaji wa lazima kwa kila mtoto anayezaliwa na kila kifo kinachotokea nchini, ikiwa ni namna ya kuziba pengo la kutokuwepo kwa vitambulisho vya taifa, ambavyo vingesaidia kupata idadi halisi ya vifo vya akina mama wanaofariki wakati wa kujifungua.  

Ahadi ya bajaji ilikuwa miongoni mwa 'ahadi za papo kwa papo za  mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) (sasa rais), Jakaya Kikwete ambaye akiwa Iringa wakati wa kampeni, aliahidi kuwa akipata ridhaa ya wananchi kuongoza kipindi cha pili, serikali yake itapambana kuzuia vifo vya akina mama wajawazito kwa kununua bajaji 400 ili zitumike kuwasafirisha kuwahi matibabu.

Ahadi hiyo ya rais, ililenga hasa maeneo ya vijijini ambako akina mama wengi wajawazito bado wanalazimika kujifungulia majumbani na kuhatarisha maisha yao, huku wengine wakifariki dunia wakati wakiwa njiani wakipelekwa vituo vya afya, kutokana matatizo ya miundombinu ya usafiri, kama vile ukosefu wa barabara, magari na umbali wa vituo vyenyewe vinavyotoa huduma hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bi. Blandina Nyoni, akikiri kutofua dafu kwa usafiri huo katika baadhi ya maeneo nchini kutokana na ubovu wa miundombinu, alisisitiza kuwa mgawo unaoendelea hivi sasa katika kusaidia suala la usafiri kwa wajawazito, halihusishi bajaji, bali pikipiki za miguu mitatu, akizisifia kuwa ni madhubuti na zinahimili mazingira ya Tanzania kwa sehemu kubwa.

Mbunge wa Kibiti, Bw. Abdul Malombwa alisema kuwa kwa mazingira ya jimboni kwake, ambako ili mtu aweze kutoka sehemu moja hadi nyingine analazimika kupanda mtumbwi, kutokana na vijiji vingi kuzungukwa na maji, matumizi ya bajaji kwa ajili ya kubeba akina mama wajawazito ni suala lisilowezekana, akipendekeza wananchi 'wake' wafikiriwe kuhudumiwa kwa boti.

Mbunge huyo alitolea mfano wa mama mmoja mjamzito ambaye alifariki akiwa njiani, akipelekwa kwenda kupata matibabu, baada ya kupanda mtumbwi ambao ungetumia saa takriban 10 kufika eneo la ambalo angepata huduma za afya wakati wa kujifungua.

Mbunge mwingine, Bi. Faida Bakari (Viti Maalum-CCM) alisema kuwa serikali inapaswa ijidhatiti kuwahudumia Watanzania kwa kutumia magari ya wagonjwa, akisema kuwa ni hatari kwa Tanzania kuiga mambo kutoka nchi zingine wakati mazingira ya hapa nyumbani hayaruhusu hatua fulani kufikiwa kabla ya hatua nyingine kupitiwa.

"Serikali ijitahidi kununua na kutumia ambulances si bajaji, matumizi ya bajaj kwa wajawazito ni hatari sana, tusipende kuiga mambo kwa sababu nchi zingine wanafanya basi nasi tufanye tu, tuwe tunaiga mambo mazuri, si kuiga mambo mabaya. Nikiwa mwanamke najisikia uchungu sana kuona akina mama wengi wanakufa wakati wa kujifungua.

"Wanaojua mama mjamzito anavyohangaika...achilia mbali wakati wa kusubiri kujifungua wakati wa uchungu, ile kusafirishwa tu ni tatizo. Mama mjamzito hawezi kukaa kitako wakati wa uchungu bali anatakiwa kulala," alisema Bi. Bakari.

Akijibu hoja za wabunge katika suala la matumizi ya bajaj na baadaye maswali ya waandishi wa habari, Bi. Nyoni alisema kuwa serikali inatambua kuwa pikipiki zinazogawiwa sasa haziwezi kukidhi mahitaji kwa kila sehemu nchini, kwa kuhimili mikimikiki ya usafiri kutokana na ubovu wa miundombinu, kwani kila eneo linatofautiana na jingine.

"Mwenyekiti, alichosema mbunge hapa (Bw. Malombwa) nakielewa alikisema hata wakati wa mjadala wa bajeti yetu bungeni na tuliahidi kulifanyia kazi...hizi tunazogawa si bajaji bali ni pikipiki za matairi matatu, ambazo zina sehemu ya kulala mgonjwa na ni very powerful (zina nguvu) kupanda milima. Na sisi tunafikiria interventions (huduma) zitajikita katika pikipiki hizi na ambulances kama wabunge walivyosema.

Akihitimisha kikao hicho cha PAC na watendaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bw. Cheyo aliitaka wizara hiyo kufanyia kazi ushauri waliopewa kutokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ambaye alibaini mapungufu mengi hasa katika ufuatiliaji wa mipango na mikakati ya kuzuia vifo vya akina mama wajwazito ambavyo bado vinaonekana kuwa juu.

Wabunge walishauri watendaji wa wizara kuacha kuzungumzia vitu vilivyoko katika makaratasi (mipango isiyokuwa na utekelezaji na takwimu zisizokuwa na uhakika), bali kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mipango hiyo kwa kila hatua, kwani Watanzania wanataka kuona vifo vya akina mama hao vinapungua na kumalizika kabisa.

No comments:

Post a Comment