25 October 2011

Aggreko yaingiza megawati 100 gridi ya taifa

Na Tumaini Makene

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Adam Malima (wa pili kulia) akisikiliza maelezo kuhusu mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Aggreco kutoka kwa Mkuu wa Operesheni wa kampuni hiyo, Bw. David Wanyaike (kulia)  wakati wa uzinduzi mitambo hiyo, Dar es Salaam jana.

WAKATI Kampuni ya Aggreko ikizindua uzalishaji wa megawati 100 za umeme kwenye gridi ya taifa kwa mkataba wa
mwaka mmoja, mzimu wa mkataba wa kampuni tata ya Richmond bado unaitisha serikali na kueleza kuukwamisha kutekeleza mpango wa dharura wa kumaliza mgawo wa umeme nchini.

Pia uongozi wa Shirika la Umeme (TANESCO) umeshindwa kuweka wazi ni fedha kiasi gani za walipa kodi zitagharimia mkataba huo kulipia uzalishaji kila siku huku mtendaji wa shirika hilo aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji akiishia kujibu kirahisi kuwa hajui, hivyo kuzua maswali mengi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa megawati hizo jana, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Adam Malima, alisema 'mambo ya Richmond' yamesababisha serikali kupitia TANESCO na Mfuko wa Huduma za Jamii (NSSF) kuwa makini kupata mitambo ya kuzalisha megawati 150 sehemu ya mpango kabambe wa kumaliza tatizo la nishati hiyo.

Bw. Malima alisema katika udharura wa sasa unaoikabili nchi kwa kupungukiwa megawati 250 hadi 300, uzalishaji wa megawati hizo 100 za Aggreko zinatia matumaini kuwa nchi haitarudi katika hali mbaya iliyokuwa imefikia mwezi Juni, Julai na Agosti.

Alisema TANESCO na NSSF walishakwenda hatua kadhaa kupata mitambo hiyo ya ufuaji umeme lakini wakalazimika kurudi nyuma ili kujipanga na kuangalia taratibu za manunuzi akisema kuwa bodi ya NSSF imelazimika kukaa kujadili suala hilo.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe alinukuliwa hivi karibuni akiweka wazi kuwa NSSF walishakwenda kuonana na muuzaji wa mitambo lakini wakakuta mambo yanayofanana na yale ya Richmond akimaanisha kampuni isiyoeleweka hivyo wakalazimika kuachana na kuanza utaratibu wa kupata mitambo mingine.

Richmond kampuni iliyoingia mkataba wa kifisadi kwa harufu ya rushwa na TANESCO kuzalisha umeme wa dharura imezua utata juu ya uwepo wake kisheria ambapo Kamati Teule ya Bunge ilibaini kuwa ni kampuni ya kitapeli ya mfukoni.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Aggreko, Bw. Kash Pandya, alidai kampuni yake kwa kutambua udharura unaoikabili nchi katika suala la umeme imeleta mitambo mingine inayoweza kuzalisha megawati 50 na kwamba iko tayari kuutumia iwapo itaombwa na TANESCO na serikali.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Uzalishaji wa TANESCO, Bw. Boniface Njombe, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo alisema Kampuni ya Aggreko ilianza kuingiza katika gridi na kuliuzia shirika hilo umeme Septemba 29, mwaka huu na kumalizia megawati zingine 50 katika mitambo yake ya Tegeta Oktoba 22 mwaka huu.

1 comment:

  1. Pesa zinazotumika kwa ajili ya malipo ya hiyo mitambo kwanini zisingetumika kwa ajili ya kununuwa mitambo yetu wenyewe?,Hivi tutaishia hivi mpaka lini?.Wajanja wachache ndio wanao kula fedha za walipa kodi.

    ReplyDelete