19 September 2011

Yanga 'mwaka wa shetani'

*Simba SC yawekewa kigingi

Na Zahoro Mlanzi

BAO lililofungwa dakika ya 20 na mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor', limerudisha majonzi kwa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga baada ya
kulala kwa bao 1-0 katika mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Yanga ilianza tambo, baada ya kuinyuka African Lyon bao 2-1 ukiwa ndiyo ushindi wake wa kwanza katika michezo minne ya ligi hiyo, lakini jana imejikuta ikiwatoa mashabiki wake uwanjani vichwa chini baada ya kukubali kipigo hicho.

Kwa matokeo Azam, sasa imefikisha pointi 11 na kushika nafasi ya pili sawa na Mtibwa Sugar, ila zinatofautiana kwa mabao ya kufungwa na kufungwa huku Yanga, ikibaki katika nafasi yake ya saba kwa pointi sita.

Katika mchezo wa jana uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Yanga itajutia nafasi nyingi ilizopata kipindi cha kwanza, ambapo washambuliaji wake hawakuwa makini kukwamisha mpira wavuni.

Dakika ya 17, Hamis Kiiza wa Yanga alikosa bao la wazi kwa kichwa, alichopiga kutoka nje akibaki na kipa Ali Mwadin Ali, akiunganisha krosi ya Nurdin Bakari.

Yanga iliendelea kuliandama lango la Azam na dakika moja baada ya shambulizi hilo, ilifanya lingine la kushtukiza wakati Shadrack Nsajigwa alipoonana vyema na Haruna Niyonzima, lakini shuti la Niyonzima lilipaa juu ya goli.

Kabla ya Yanga kuwabana Azam kuanzia dakika ya 17, Azam ilikuwa ya kwanza kubisha hodi langoni mwa Yanga baada ya Mrisho Ngassa, kuunganisha vibaya krosi ya Khamis Mcha na mpira kutoka nje.

Dakika ya 20, Adebayor aliifungia Azam bao pekee la ushindi baada ya kuwazidi mbio mabeki wa Yanga, Chacha Marwa na Mohamed Mbegu kutokana na pasi iliyopigwa na Ibrahim Mwaipopo, aliyeunasa mpira kutoka kwa Shamte Ally wa Yanga na moja kwa moja mpira kujaa wavuni.

Kipindi cha pili, Yanga ilianza kwa kasi na dakika ya 62, Rashid Gumbo aliyeingia badala ya Pius Kisambale, alipiga shuti nje ya eneo la hatari na kupaa juu akimalizia pasi ya Nsajigwa.

Naye Mwandishi Wetu, anaripoti kutoka Bukoba kwamba vinara wa ligi hiyo Simba, jana waliwekewa kingi na Kagera Sugar baada ya kulazimishwa bao 1-1 katika mechi iliyopigwa Uwanja wa Kaitaba.

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza bao kipindi cha pili kupitia kwa Patrick Mafisango, lakini kabla ya bao hilo Felix Sunzu alikosa penalti. Kagera Sugar ilisawazisha dakika ya 75 kupitia kwa Hussein Swed kwa mkwaju wa penalti.

Kwa matokeo hayo, Simba bado inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 14.

1 comment:

  1. Vipi Timbe uwanja bado mbaya pia?au mwamuzi alipendelea.Tueleze tu tujue.Au ligi ndio kwanza imeshaanza?

    ReplyDelete