19 September 2011

'Walimu mnaotaka kujiendeleza kielimu toeni taarifa mapema'

Na Yusuph Mussa, Lushoto

WITO umetolewa kwa walimu wanaotaka kujiendeleza kielimu, kutoa taarifa mapema katika mamlaka husika wanapoomba nafasi za kwenda kusoma ili wasiathiri masomo kwa
wanafunzi.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 14 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Kongei, iliyo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Bw. Lucas Kalombola, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Lushoto mkoani hapa.

Bw. Kalombola ambaye ni mtaalamu wa madini viwandani (IML),
aliwataka wazazi kutoa fursa sawa za elimu kwa watoto wa kike na kiume kwani katika karne hii, mazingira ya kazi hayabagui jinsia.

Aliwataka wanafunzi shuleni hapo kusoma kwa bidii ili wajiwekee msingi mzuri wa maisha kwa siku za usoni.

Mwakilishi wa wazazi Bi. Catherine Singano, alisema lazima wazazi walipe ada na gharama nyingne kwa wakati ili kuboresha kiwango cha elimu na kuongeza ufaulu shuleni hapo.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Bi. Imelda Mchome, alisema shule inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ukumbi wa mikutano, nyumba za walimu na mabweni.

Mwisho.
6666666

LEAD:
Pinda: Tamwimu matumizi vocha
za pembejeo zinanipa mashaka
Na Grace Michael, Mara

WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda, ameonesha wasi wasi wake juu ya takwimu za matumizi ya vocha za pembejeo mkoani hapa hatua iliyomfanya atoe agizo la kuwepo kwa daftari la mkulima ili kupata takwimu zenye ukweli.

Bw. Pinda alitilia shaka takwimu hizo juzi akiwa ziarani mkoani Mara baada ya kusomewa taarifa ya Mkoa ambazo zilionesha vocha hizo kutumika ipasavyo na kunufaisha walengwa.

“Kwa mujibu wa taarifa yenu, mna jitihada kubwa katika eneo la vocha lakini sitaki kuamini hizi takwimukwa sababu eneo hili lina wizi mkubwa na limejaa wajanja.

“Sidhani kama na nyie hamuusiki katika hili, msimu ujao hakikisheni mnafuatilia kwa karibu ili kujiridhisha kama kweli walengwa wananufaika na vocha hizo,” alisema Bw. Pinda.

Alisema ili takwimu hizo ziwe za ukweli, lazima kila Wilaya na Mkoa uwe na daftari la wakulima ili wamelima zao gani, ukubwa wa eneo lake na matumizi ya pembejeo.

Aliongeza kuwa, eneo la vocha linaonekana kuchakachuliwa kwa kiwango kikubwa ambapo Serikali imelazimika kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua eneo hilo.

Akizungumzia kilimo mkoani humo, Bw. Pinda alisema bado hakina tija ya kutosha ndio sababu kubwa iliyomfanya awe na mashaka na takwimu za vocha.

Aliwataka viongozi kuhakikisha wanahamasisha wananchi kutumia zana bora za kilimo na kusisitiza matumizi ya wanyama katika kilimo ili kiwe na tija inayotakiwa.

“Kila siku nasisitiza matumizi ya matrekta madogo kwa kuwa hili ndio jembe la mkulima, kinachoonekana matumizi yake ndiyo yanakosewa hivyo hakikisheni kama Mkoa, mnakuwa na wataalam ambao watatoa mafunzo kwa wakulima kabla ya kuyatumia,” alisema.

Aliwataka Wakurugenzi wa halmashauri zote, kuwa wabunifu katika kuwasaidia wananchi wao ili watoke hapo walipo na kuwataka wafugaji, kuangalia uwezekano wa kupungumza idadi ya mifugo waliyonayo ili iendane na eneo la malisho.

Wakati huo huo, Bw. Pinda Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wasiojua kipato halisi cha wananchi wao hawafai kuwa viongozi katika maeneo waliyopo.

Alisema kiongozi mzuri lazima afahamu viashiria mbalimbali kama hali za wananchi na maendeleo yao ili atambua namna ya kuwasaidia ili kujikwamua na hali ngumu za maisha.

“RC, DC DED na vingozi wengine ambao hawajui pato la mwananchi ili kupima ubora wa maisha yao, hawafai hata kidogo, jifunzeni kutathimini hali za wananchi wenu,” alisema.

Alisema kuwa Mkoa huo ni wa 14 kati ya 21 ambapo wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka ni sh. 642,000 ambazo kama zitagawanywa kwa mwezi au siku, kipato hicho ni kidogo ukilinganisha na mikoa mingine inayowazunguka.

“Mkoa wa Arusha kipato cha mwananchi kwa mwaka sh. 950,000, Mwanza 830,000 hivyo lazima mtafakari kwa nini mnakuwa nyuma ya hao majirani zenu huku mkiwa na fursa nyingi kuwazidi hao, fanyeni kazi ya ziada kuhakikisha mnatumia vyema rasilimali zilizopo ili mpige hatua inayostahili,” alisema Bw. Pinda.

Bw. Pinda alikwenda mbali zaidi na kusema Mkoa huo haukuwa na sababu kuomba msaada wa chakula serikalini kwani takwimu zinaonesha walizalisha zaidi lakini hawakuwa na nidhamu katika matumizi ya chakula hicho.

No comments:

Post a Comment