Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga leo, inatupa karata nyingine kwa African Lyon katika mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaopigwa
Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na matokeo ya msimu uliopita, ambapo timu hizo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare katika michezo yote miwili waliyokutana msimu huo.
Lakini presha zaidi itakuwa kwa Yanga, ambayo tangu kuanza kwa msimu huu imeandamwa na mikosi ya kushindwa kufanya vyema katika michezo ya awali baada ya kutoka sare tatu na kufungwa mmoja.
Yanga ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na JKT Ruvu na kutoka sare tatu na timu za Moro United, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting kitu kilichozua maswali mengi kwa mashabiki na wanachama wa klabu.
Lyon yenyewe ambayo ipo nafasi ya saba kwa pointi tano ikiwa imeshinda mchezo mmoja, sare mbili na kufungwa mmoja hivyo itashuka uwanjani kuwadhihirishia wapinzani wao kwamba msimu huu ni kushinda michezo yao.
Timu hiyo ilianza vibaya ligi hiyo kwa kufungwa na Coastal Union ya Tanga bao 1-0, ikatoka sare na Toto African ya bao 1-1, ikaifunga Azam FC bao 1-0 na kumalizia na Polisi Dodoma kwa suluhu.
Kwa matokeo hayo ni dhahiri Lyon, hadi sasa imepata matokeo mazuri zaidi ya Yanga, hivyo itakuwa katika nafasi ya kuibuka na ushindi, endapo itajipanga vizuri.
Akizungumzia mchezo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema wana uhakika watafanya vizuri katika mchezo huo, baada ya kikao na viongozi wa matawi kilichofanyika wiki hii, hivyo kazi ni moja katika mchezo huo.
No comments:
Post a Comment