15 September 2011

Simba 'yatafuna Polisi Chamazi'

*Yang'ang'ania kileleni

Na Sepeciroza Joseph

MABINGWA wa ngao ya Jamii, Simba, baada ya kuonja utamu wa kuongoza Ligi Kuu msimu huu, jana iling'ang'ania kileleni baada ya kuichapa
Polisi Dodoma bao 1-0, katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi Jijini Dar es Salaam.

Simba ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao dakika ya kwanza, lililofungwa na Gervais Kago kwa shuti kali lililomshinda kipa Agathon Kwanduko na mpira kujaa wavuni.

Vinara hao wa ligi hiyo wakicheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo, unaomilikiwa na Klabu ya Azam FC, ulijaza watazamaji kuzidi mechi zote zilizowahi kuchezwa kwenye Uwanja huo, licha ya kupandisha viingilio.

Polisi Dodoma, walibadilika na kuliandama lango la Simba, dakika ya 16 ambapo Kulwa Mobby, alipata nafasi nzuri na kupiga shuti kali lililotoka nje ya lango.

Bantu Admini na Mobby walikuwa wakionana vizuri na kuisumbua ngome ya Simba, lakini kila walipojaribu kufunga, kipa Juma Kaseja alikuwa makini kuhakikisha nyavu zake hazitikiswi.

Dakika ya 50 na 56, Emmanuel Okwi alipata nafasi nzuri ya kufunga, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango la Polisi Dodoma, huku Jerry Santo akishindwa kuzifumania nyavu wakati akiwa na nafasi nzuri ya kufunga.

Kwa matokeo hayo, Simba imezidi kujichimbia kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa na pointi 13, huku ikiipeleka mkiani Polisi Dodoma kwa kuwa na pointi tatu, lakini ikizidiwa na Yanga kwa uwiano wa mabao.

Kituko kilichojitokeza uwanjani hapo ni kwamba mashabiki wa Simba, tayari wamejichagulia eneo lao la kukaa na kuwaachia watani wao Yanga, sehemu nyingine, kama ilivyo katika viwanja vya Taifa na Uhuru, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Simba, Moses Basena alisema vijana walikosa umakini kila walipokuwa wakilifikia lango la wapinzani wao.

Basena alisema, amefurahi kuzoa pointi zote tatu katika mechi hiyo, hivyo wanajipanga kuhakikisha mechi zitakazofuata wanashinda, ili kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Polisi Dodoma, Joseph Kanakamfumu alisema wamepoteza mechi ya jana, kwa sababu wachezaji wake walikosa umakini kila walipofika langoni mwa Simba.

"Kikosi changu kimecheza kwa kiwango cha juu muda wote na kufanikiwa kuwabana wapinzani wetu, lakini umakini ndiyo uliotuangusha," alisema Kanakamfumu.

Pia katika mchezo huo ulinzi ulikuwa wa kutosha, huku mashabiki wakiingia na kutoka uwanjani kwa busara, kuliko inavyokuwa katika viwanja vingine vya Dar es Salaam.

Simba: Juma Kaseja, Nasor Said/Shomari Kapombe, Juma Jabu, Juma Nyoso, Victor Costa, Patrick Mafisango, Ulimboka Mwakingwe/Uhuru Seleman, Jerry santo, Felix Sunzu, Gervas Kago/Haruna Moshi 'Boban', Emmanuel Okwi.

Polisi Dodoma: Agathon Mkwanduko, Salmin Kissikissi, Nasor Mhagama, Frank Sindato, Elias Maftah, Ibrahim Masawe, Bryton Mponzi, Haruna Hassan/Delta Nyamanche, Kulwa Mobi, Hamad Kambangwa/Sihaba Mkude, Bantu Admin.

No comments:

Post a Comment