28 September 2011

Yanga, Coastal kiama leo

Na Zahoro Mlanzi

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo inatupa karata yake nyingine Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuumana na Coastal Union ya Tanga katika
mfululizo wa mechi za ligi hiyo.

Mabingwa hao watakuwa na kibarua kigumu, watakapoikaribisha timu hiyo ambapo mara nyingi kufungwa na timu kubwa huwa ni ngumu na ndiyo maana hata vinara wa ligi hiyo, Simba waliifunga kwa shida bao 1-0.

Yanga imekuwa na mwendo wa kusuasua katika ligi hiyo, hali iliyoifanya mpaka sasa kupoteza michezo miwili dhidi ya JKT Ruvu na Azam FC na kuambulia pointi tisa kutokana na michezo saba iliyocheza huku ikiwa katika nafasi ya nane.

Mbali na matokeo hayo mabaya, ambayo yanaweza kufananisha na timu ya Arsenal ya Uingereza ambayo nayo imeanza msimu vibaya, kwani hadi sasa imeshinda michezo miwili dhidi ya Villa Squad kwa mabao 3-2 na African Lyon 2-1 na iliyobaki ilitoa sare.

Kwa upande wa Coastal Union, yenyewe inashika mkia ikiwa na pointi nne kutokana na michezo saba iliyocheza ambapo ilifanikiwa kushinda mchezo mmoja, dhidi ya African Lyon kwa bao 1-0 na kutoa sare na Mtibwa Sugar ya Morogoro ya bao 1-1 na iliyobaki imepoteza.

Pamoja na matokeo hayo ya Yanga, lakini imekuwa katika kipindi kizuri hususani baada ya kurejea kwa beki wake mahiri, Nadir Haroub 'Canavaro' ambaye alikuwa muda mrefu majeruhi na katika mchezo uliopita alicheza.

Akizungumzia mchezo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe alisema mchezo huo utakuwa mgumu ikizingatiwa Coastal ni timu ya siku nyingi katika ligi hiyo, hivyo kutakuwepo na ushindani mkubwa.

Alisema wachezaji wapo katika morali nzuri, ikizingatiwa na ushindi walioupata dhidi ya Villa, umeleta hali mpya hivyo hakuna shaka watahakikisha wanashinda mchezo huo, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufukuzia ubingwa wao.

Naye Ofisa Habari wa Coastal, Edo Kumwembe akiuzungumzia mchezo huo alisema, Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wenye uzoefu tena wa kimataifa, lakini watahakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.

Katika mchezo huo, viingilio vilivyopangwa ni sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa. VIP C ni sh. 7,000, VIP B ni sh. 10,000 na VIP A itakuwa sh. 15,000.

No comments:

Post a Comment