28 September 2011

Rooney hatihati kuivaa Montenegro

LONDON, Uingereza

MSHAMBULIAJI Wayne Rooney, amebakia kwenye hatihati kucheza mechi ya kuwania kufuzu mashindano ya Kombe la Ulaya, Euro 2012 ya ugenini dhidi ya Montenegro
ambayo itaamua hatima ya England, limeripoti gazeti la Mirror.

Rooney jana alikosa kucheza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, dhidi ya FC Basel ya Uswisi huku kocha Sir Alex Ferguson, akishindwa kueleza kama anaweza kucheza Jumamosi katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya
Norwich itakayopigwq katika Uwanja wa Old Trafford.

Ingawa Rooney alishindwa kufanya mazoezi katika Uwanja wa United Jumatatu, kocha Ferguson na benchi lake la ufundi hawataki kumwahisha kucheza baada ya kuumia msuli wa paja, ambao ulikuwa umekaza.

Rooney anaweza kukosa kucheza mechi ya Jumamosi dhidi ya Norwich wikiendi, kitu ambacho kinaweza kufanya akaachwa pia kwenye kikosi cha Fabio Capello, kitakachocheza dhidi ya Montenegro Oktoba 7 mwaka huu.

Alipoulizwa kuhusu hali ya Rooney, baada ya mechi kati ya United dhidi ya Stoke City, Jumamosi iliyopita kwa matokeo ya bao 1-1, Ferguson alisema hatacheza dhidi ya Basel.

Alisema maumivu ya msuli husumbua lakini wanatumaini anaweza kurejea uwanjani haraka.

Rooney alitarajiwa kuwa miongoni mwa nyota wanane wa United, ambao walikosa mechi ya jana ya Kundi C dhidi ya Basel, kutokana na umajeruhi.

Ferguson alimkosa pia Javier Hernandez 'Chicharito', ambaye ni majeruhi wa mguu aliogongana na kipa Asmir Begovic.

Mlinzi Chris Smalling na Jonny Evans, nao ni majeruhi huku Nemanja Vidic aliyeumia katika mchezo dhidi ya West Brom, hajaanza mazoezi.

No comments:

Post a Comment