16 September 2011

Wengi la Saba wakosa ujuzi kusoma, kuandika

Na Tumaini Makene

UTAFITI umebaini kuwa watoto wengi wakiwemo wa Darasa la Saba, wanamaliza elimu ya msingi wakiwa hawana stadi za msingi za ujifunzaji kusoma, kuandika na
kuhesabu.

Utafiti huo uliofanywa nchi nzima, umebaini kuwa ni watoto watatu pekee kati ya 10 wa Darasa la III na wanne kati ya saba wa Darasa la VII, ndio wanaoweza kusoma Kiswahili 'cha' Darasa la II huku pia wengi wao wakishindwa kusoma Kiingereza,
kufanya hesabu za kutoa, kujumlisha na kuzidisha za ngazi hiyo ya darasa la pili.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya tathmini ya elimu kwa mwaka 2011, iliyowasilishwa na Mratibu wa Utafiti wa Uwezo,  Dkt. Grace Soko, nusu ya watoto wa Darasa la VII, ndiyo pekee wanaweza kufaulu masomo ya Hesabu, Kiswahili na Kiingereza, ya kiwango cha Darasa la II.

Katika ripoti hiyo iliyozinduliwa jana Dar es Salaam, mbele ya wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, pia imebainishwa kuwa ni mtoto moja pekee kati ya 10
wa Darala la III anaweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya Darasa la II, huku pia baadhi ya watoto wa Darasa la Saba nao wakishindwa kusoma na kujibu maswali yanayotokana na hadithi ya lugha hiyo katika kiwango hicho cha darasa la la pili.

Utafiti huo ambao ulifanywa Mei, mwaka huu, kwa kutumia sampuli nasibu katika kupata washiriki, ulihusisha wilaya 132 nchi nzima, vijiji 30 kwa kila wilaya, kaya 76, 796, ambapo watoto 128, 000, walifanyiwa tathmini hiyo ya uwezo wao wa kusoma Kiswahili, Kiingereza na kufanya Hisabati.

Mapungufu makubwa matano yaliyobainishwa katika utafiti huo ni kuwa, watoto watatu pekee kati ya 10 wa darasa la tatu wanaweza kusoma hadithi ya Kiswahili, mtoto mmoja
pekee kati ya 10 wa darasa la tatu anaweza kusoma hadithi rahisi ya kingereza.

Kwa mujibu wa utafiti huo wanafunzi watatu kati ya 10 wa darasa la tatu wanaweza kujumlisha, kutoa na kuzidisha hesabu za darasa la pili, watoto wa Kitanania wanajifunzia katika mazingira yenye utofauti wa kiusawa na mwisho ni kuwa walimu wanatumia muda mwingi nje a shule.

Katika tathmini ya elimu kwa mwaka 2010 ya Uwezo, ilibainika kuwepo kwa ufaulu mdogo katika kusoma na kuhesabu nchi nzima.

Uwezo wa watoto ulikuwa mdogo hasa katika somo la Kiingereza, ingawa hata hivyo kiwango cha uwezo kilitofautiana kutoka wilaya moja hai nyingine.

Katika somo la Kiingereza, ripoti hiyo inasema "Kama ilivyo katika somo la  Kiswahili, kila mtoto wa Darasa la Tatu, anapaswa kujua kusoma Kiingereza cha Darasa la Pili, lakini kama ilivyokuwa kwenye Kiswahili,  awamu hii ikiwa zaidi, watoto wengi hawakuweza kusoma Kiingereza, wakiwemo wa Darasa la Saba.

Katika somo la Hesabu, ni watoto watatu pekee kati ya 10, wa Darasa la Tatu wanaweza kufanya hesabu za kujumlisha, kutoa na kuzidisha, ambapo pia imebainika kuwa
kuzidisha kunawapatia tabu zaidi wanafunzi, wakiwemo wa Darasa a Saba pia waliopata shida kumudu hesabu za Darasa la Pili.

Utafiti huo pia umebaini kuwepo kwa athari za tofauti za kimaisha, kijamii na kiuchumi katika uwezo wa wanafunzi shuleni, ambapo watoto wa Tanzania wanajifunza katika mazingira yenye utofauti wa kiusawa, wale wa mijini wameonekana kufanya vizuri kuliko wenzao wa vijijini.

Utafiti pia umebainisha kuwa walimu wengi hawatumii muda wao kuwa shuleni, ambapo walimu wanne kati ya watano ndiyo walikuwa shuleni wakati watafiti wa Uwezo walipofika shuleni, huku pia shule tisa kati ya 10 zilizofanyiwa tathmini zilikuwa
angalau mwalimu mmoja ambaye hakuwepo shuleni siku ya utafiti.

1 comment:

  1. Katika mfumo wa elimu wa aina hii wa Elimu, ndiko eti tunategemea kupata: madereva, manahodha, wataalamu mbalimbali, wanasiasa na raia wema kisha tuweze kushindana katika uchumi wa Afrika Mashariki na Dunia; Itawezekanaje?
    Hakuna sekta muhimu (popote) kama ELimu na Afya. Na huko kunapoharibika kama ilivyo Tanzania, basi ni hakika kuwa, hakuna Idara yoyote itakayosalimika. Kote kunaoza, ukiwemo utamaduni wetu.

    ReplyDelete