13 September 2011

Wazamiaji kimataifa watua visiwani Z'bar

*Watachunguza meli iliyozama baharini
*Kamati ya Bunge yatinga kutaka maelezo
*Tume huru kuundwa kuchunguza chanzo
*JK aeleza alivyopokea taarifa ya ajali


Na Waandishi Wetu, Zanzibar

WAZAMIAJI 12 kutoka nchini Afrika ya Kusini, wamewasili mjini Zanzibar wakiwa na
zana za kisasa za uzamiaji, ambapo wataungana na wazamiaji wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Bw. Aboud Mohammed Aboud, alisema wazamiaji hao waliowasili juzi usiku kuchunguza meli kujua kama bado kuna miili iliyokwama ndani ya meli ya Mv Spice Islander iliyozama chini ya bahari eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

"Wazamiaji hawa wamewasili wakiwa na zana za kisasa za uzamiaji kazi ya kwanza itakayofanywa na timu hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaifikia meli hiyo iliyozama umbali wa karibu nusu kilometa kwenye mkondo mkubwa wa maji na majabali," alisema.

Alisema kuwa bado Serikali na wananchi mbalimbali wanadhani kuna miili ya watu waliokwama katika vyumba vya meli hiyo tangu ilipozama usiku wa Jumamosi Septemba 10 mwaka huu ikiwa na idadi ya abiria isiyojulikana.

Bw. Aboud alisema tangu walipookolewa abiria 619 na kuopolewa kwa miili ya watu 197 hadi juzi jioni, hawajaokolewa watu wengine ama mwili wa abiria aliyekufa maji.

Wakati huo huo Waziri wa Uchukuzi Bw. Omari Nundu ametoa salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki kutokana na ajali ya  Meli ya Mv Spice Islander.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es salaam jana waziri huyo na aliwapa pole wafiwa wote pamoja na kuwaombea afya njema wale wote walionusurika  katika ajali hiyo.

"Tumepokea kwa masikitiko makubwa sana  na tunawapa pole wale wote waliopotelewa na ndugu zao,tunamwomba mwenyezi mungu awafariji katika kipindi hichi kigumu,"ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Naye Martha Fataely anaripoti kutoka Siha kuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Kaskazini,limeitaka serikali kuchunguza kwa kina chanzo cha ajali ya meli ya Spice Islander kwa kuwa kuna dalili za uzembe wa baadhi ya watendaji.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Saba wa KKKT jimbo la Siha,Askofu Mkuu wa Dayosisi hiyo Dkt. Martin Shao alisema taifa limekuwa likipoteza mamia ya wananchi wake katika ajali mbalimbali na sasa ipo haja ya kukomesha ajali hizo.

Alisema matukio mengi ya ajali husababishwa na uzembe wa baadhi ya watu lakini hawachukuliwi hatua ipasavyo ili kuwa fundisho kwa watu wengine hivyo aliiomba serikali kuangalia upya namna ya kushughulikia na kufuatilia vyanzo vya ajali hizo.

Aidha katika hatua nyingine Askofu Shao aliiomba serikali kupitia vyombo vyake kuthibiti matukio hayo kwa kufuatilia kwa karibu usalama wa vyombo hivyo vya usafiri kwa asilimia kubwa havifanyiwi ukarabati unaokidhi na hivyo kusababisha adha kubwa kwa watu.

“Kutokana na upungufu wa askari wa usalama barabarani uliopo baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kukiuka taratibu za usafirishaji na hivyo kuhatarisha maisha ya wengi,”alisema.

Alisema ni vyema kwa serikali kuchukua hatua kwa kutoa mamlaka kwa viongozi wengine wakiwemo wa vijiji na kata katika kusimamia sheria za usalama barabarani sanjari na kuvitolea taarifa vyombo vinavyoonekana kutokuwa na usalama kwa watumiaji.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakijali upatikanaji wa fedha badala ya maisha ya Watanzania walio wengi na wanaotumia vyombo hivyo vya usafiri kwani huweka vifaa chakavu na feki katika vyombo hivyo bila kujali athari zake.

Hata hivyo askofu huyo aliomba pia kudhibiti taratibu za utoaji na upatikanaji wa leseni kwani kwa sasa hutolewa bila kufuata taratibu zilizowekwa na serikali huku kukiwa hakuna mfuatiliaji wa leseni hizo.

Pamoja na mambo mengine katika mkutano huo unaofanyika katika kituo cha wanawake cha Angaza wilayani Siha, dayosisi hiyo imetoa msaada wa sh. mil 1.5 kwa serikali kwa ajili ya kusaidia waliopatwa na maafa katika ajali ya meli hiyo. Msaada huo ulikabidhiwa kwa mkuu wa wilaya ya Siha,Bi. Anarose Nyamubi.


JK aeleza masikitiko

RAIS Jakaya Kikwete, ametoboa siri ya moyo wake kuhusu ajali hiyo na kuweka wazi kuwa ilimpa mshtuko wa hali ya juu baada ya kupigiwa simu na Mkuu wa Majeshi Generali David Mwamunyange, saa 9.00 usiku akimpa taarifa hiyo.

"Ninachoshukuru ni kwamba Mkuu wa majeshi wakati ananipa taarifa aliniambia tayari wameshatuma wanajeshi kwenda kuanza kuokoa watu, nilishtuka sana,"alisema Rais Kikwete.

Kamati ya uchunguzi

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema matayarisho ya kamati ya kuchunguza meli iliyozama ya MV Spice Islanders yanakwenda vizuri na wakati wowote itatangazwa kamati hiyo.

Hayo yameelezwa na Makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, wakati akipokea msaada wa sh. milioni tano kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe.

Balozi Seif alisema serikali itakuwa makini katika uchunguzi huo ili ukweli uweze kupatikana na kuahidi kuwa haitasita kuchukuwa hatua iwapo itabainika kufanyika kwa uzembe kabla ya tukio hilo.

“Tume itaundwa kuchunguza kwa umakini sana na tunatarajia kuitangaza wakati wowote,” alisema Balozi Seif.

Licha ya Bw. Mbowe Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) tawi la Zanzibar pia ilitoa msaada wa katoni 60 za maji na kukabidhiwa na Meneja wa tawi hilo Bw. Rajab Ramia.

Bw. Ramia alisema Benki hiyo ipo tayari kukutana na serikali kuangalia mpango wa kusaidia yatima waliotokana na ajali hiyo ili waweze kuendelea na masomo baada ya kuondokewa na wazazi wao.

Taasisi nyengine zilizotoa msaada jana ni Jumuiya ya Alyaamini kupitia Makamu Mwenyekiti wake Bw. Sharif Mohammed Juda,  waliotoa sh. milioni 15 kwa kushirikaiana na jumuiya DYCCC ya Tanzania Bara.

Alisema kwamba Jumuiya hiyo imeanzisha namba zitakazotumika kwa huduma ya M PESA, TIGO PESA na Z PESA kupitia namba 0777 41 55 60, 0719 95 69 00 na 0767 71 86 87 kwa ajili ya  kuchangia mfuko wa maafa.

CRDB watoa msaada

Benki ya CRDB pia ilikabidhi msaada wa sh. milioni 10
zilizowasilishwa na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiki wa benki hiyo Bi. Tully Mwambapa.

Alisema CRDB imeguswa na maafa hayo na kwamba kama sehemu ya jamii imeamua kutoa mchango wa sh. milioni 10 kusaidia waathirika hao.

UVCCM nao watoa msaada

Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) pia ilitoa msaada wa  sh. 600,000 huku Kanisa Anglikana pia ikitoa sh. 500,000 na Umoja wa Kiislamu Uchumi na Maendeleo pia ukitoa sh. 300,000.

Pia Spika wa Baraza la Wawakilishi Bw. Pandu Ameir Kificho, naye alitoa mkono wa rambi rambi kw Rais wa Zanzibar baada ya kukutana ghafla na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kikao kilichofanyika jana Chukwani Zanzibar.

Bw. Kificho alisema wawakilishi wanauona msiba huo ni wa taifa na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na maombolezo.

“Tumuombe Mwenyezimungu awape nguvu, afya njema na maisha marefu wananchi wenzetu waliokolewa katika ajali hiyo, waliofariki awajalie makaazi mema peponi,” alisema Bw. Kificho.

Kamati ya Bunge yatinga ZNZ


Wakati huo huo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasili mjini Zanzibar ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw.Edward Lowasa, kuungana na watanzania katika msiba huo mzito.

Licha ya maombolezo Kamati hiyo ililazimika kukutana na taasisi kadhaa ya sekta ya usafirishaji Zanzibar ikiwemo Mamlaka ya Usafiri Baharini na Bandari baada ya kukosa majibu ya kuridhisha kutoka kwa uongozi wa Polisi Zanzibar.

Kamati hiyo ilitaka kujua sababu za abiria kuzidi kiwango katika meli wakati kuna wakaguzi wa abiria ambao hutakiwa kukagua meli kabla ya kuondoka bandarini.

Kamati hiyo pia ilitaka kujua ni jinsi gani meli hiyo iliruhusiwa kuondoka ikiwa imebeba mzigo mkubwa ikiwemo abiria hivyo kusababisha vifo vya watu wasio na hatia.

No comments:

Post a Comment