21 September 2011

Wanawake wakiwezeshwa watakuza kilimo JK

Na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete, amesema wanawake wanaweza kuongeza kiwango cha uzalishaji na kukuza kilimo katika nchi zinazoendelea iwapo watapewa uwezo wa
kumiliki ardhi na kupata mikopo nafuu.

Rais Kikwete alisema hayo juzi mjini New York Marekani katika mjadala juu ya wanawake na kilimo, kuongeza hali ya usalama wa chakula Duniani mjadala uliongozwa na Waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Bi.Hilary Clinton.

"Wanawake ndio wanaofanya kazi kubwa katika kilimo, lakini hawana sauti kwa kuwa hawamiliki ardhi wala hawana uwezo wa kifedha kuongeza kipato chao,"alisema Rais Kikwete.

Omeongeza kuwa ili kuondoa hali hiyo kunahitajika mabadiliko makubwa ya sheria na sera ambazo zitahakikisha wanawake wanamiliki ardhi n apia wanawezeshwa kupewa mikopo.

Alisema suala la wanawake kupewa kipaumbele katika kilimo na kutambua mchango wao ni moja ya juhudi muhimu katika kuongeza uzalishaji na kuinua kilimo katika nchi zinazoendelea.

Alisema kutokana na hali halisi ya uchumi kwa sasa katika nchi mbalimbali mabadiliko yanayoendelea duniani ni wakati muafaka wa kutambua juhudi hizo za wanawake na kuzipa nguvu kwa kutumia elimu ili kuelimisha jamii umuhimu na mchango wao kimaendeleo.

Mapema akiwakilisha mada kuhusu wanawake na kilimo Waziri Clinton alimsifu Rais Kikwete kuwa mmoja wa voingozi katika nchi zinazoendelea ambaye anatilia mkazo kilimo na kusisitiza kutilia maanani juhudi za wanawake katika kilimo nchini Tanzania.

"Hili ni suala la kiuchumi ni jambo linalowezekana, wapo viongozi katika nchi zinazoendelea kama Rais Kikwete wanaoweka kipaumbele katika kilimo na kutilia mkazo uwezeshwaji wa wanawake kutambua juhudi zao za uzalishaji, ni jambo linalowezekana na hili ni jambo la kiuchumi sio la kijinsia,"alisema Bi. Clintoni.

Marekani imetoa kiasi cha dola milioni tano kwa ajili ya kukuza usawa katika kilimo, belimu na utafiti zaidi ili kuwepo na uwezo wa wanawake wengi zaidi waongeze uzalishaji katika kilimo.

Rais Kikwete yuko mjini New york Marekani kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaofanyika kila mwaka ambapo anatarajiwa kuhutubia baraza Kuu la Umoja Mataifa kesho na kushiriki kikao cha Baraza kuu kitafunguliwa rasmi leo.

Mbali na kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Rais Kikwete alihudhuria mikutano mbalimbali ambayo amelikwa kama Rais wa Tanzania na pia katika nyadhifa zake mbalimbali kama Mwenyekiti wa jitihada za viongozi wa Afrika katika kupambana na Malaria (ALMA).

No comments:

Post a Comment