21 September 2011

Simba, Toto kazini Yanga yasaka amani

Na Zahoro Mlanzi

MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, unaendelea tena leo kwa kupigwa michezo mitano katika viwanja vitano tofauti,  huku macho na masikio
yakielekezwa kwa mabingwa watetezi timu ya Yanga, itakayojitupa Uwanja wa Azam Chamazi na vinara wa ligi hiyo, Simba ambao wenyewe watakuwa jijini Mwanza.

Wakati miamba hiyo ya soka ikiwania pointi tatu muhimu, Azam FC itakuwa ikiiombea mabaya Simba ipoteze mchezo huo na wao kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa idadi kubwa ya mabao ili ikwee kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kuwiana kwa pointi 14, sawa na Simba.

Mashabiki wengi wa soka nchini hususan wa Jiji la Dar es Salaam, watayasubiri kwa hamu kubwa, matokeo yatakayopatikana pale Yanga itakapoumana na Villa Squad 'Watoto wa Magomeni', kutokana na mabingwa hao kutofanya vizuri katika michezo ya awali.

Yanga ambayo kwa sasa ina pointi sita katika nafasi ya tisa, ikishinda mchezo mmoja dhidi ya African Lyon na kutoka sare na Mtibwa Sugar, Moro United na Ruvu Shooting na kufungwa na JKT Ruvu na Azam FC.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sam Timbe, akiizungumzia timu yake jinsi inavyocheza hivi sasa mara baada ya kuchapwa na Azam, alisema amewafundisha kila kitu wachezaji wake, hasa safu ya ushambuliaji, lakini tatizo linabaki kwa wachezaji wenyewe kuongeza vitu vya ziada.

Akizungumzia mchezo wa leo, alisema ni mgumu na wachezaji wake wanatakiwa kuwa makini, hasa katika kipindi hiki kigumu walichonacho ili kurudisha imani kwa mashabiki wao na wanachama.

Villa Squad ipo nafasi ya pili kutoka mwisho, ikiwa na pointi nne, baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare moja, huku kupoteza mechi nyingine.

Shughuli nyingine itakuwa  Uwanja wa CCM Kirumba, ambapo vinara Simba, watakaribishwa na Toto African, katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo, hasa Toto inapokuwa nyumbani haikubali kufungwa kirahisi.

Simba, mpaka sasa hawajapoteza mchezo wowote na wapo kileleni kwa pointi 14, huku Toto ikiwa ya sita kwa kufikisha pointi nane, hivyo haitakubali kufungwa kwani itataka ishinde ili isogee mbele zaidi.

Mechi nyingine zitapigwa katika uwanja wa CCM Mkwakwani, wenyeji Coastal Union wataikaribisha Azam FC, kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa JKT Oljoro na Mlandizi, Pwani, Ruvu Shooting itaumana na African Lyon.

No comments:

Post a Comment