18 September 2011

Wanaowapa fedha ombaomba kukiona

Na Willbroad Mathias

UONGOZI wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, umetishia kuwachukulia hatua watu wanaowapa fedha ombaomba katika mitaa mbalimbali ya manispaa hiyo.Mwanasheri Mkuu wa
Manispaa hiyo, Bw. John Paul, aliyasema hayo Dar es Salaam juzi katika operesheni ya kukamata ombaomba ambao wanasababisha kero kwa wananchi.

Alisema kitendo kinachofanywa na wasamalia kuwapa fedha, kinachangia ongezeko la ombaomba mitaani.

Aliongeza kuwa, njia mbadala ya kuwasaidia ombaomba ni kupeleka fedha hizo Msikitini na Kanisani kama sadaka ili zitangazwa kuwa sadaka hiyo ni kwa ajili ya kuwasaidia ombaomba.

“Tutaweka askari wetu ambao watawajibika kukamata wasamalia wanaowapa fedha ombaomba kwani ndio wanachangia watu hawa waendelee kuwepo mitaani,” alisema Bw. Paul.

Akizungumzia oparesheni hiyo, alisema Agosti mwaka huu manispaa hiyo ilitangaza kupitia vyombo vya habari juu ya mkakati walionao ili kuondoa kero katika mitaa mbalimbali ya manispaa hiyo.

Bw. Paul alisema siku ya kwanza ya operesheni hiyo, walifanikiwa kukamata ombaomba 70, kati yao 25 ni watu wazima na waliobaki ni watoto wenye umri mdogo.

Alisema utitiri huo wa watoto unasababishwa na wazazi wao ambao wamekuwa wakiwatumikisha katika kazi hiyo jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

Aliongeza kuwa, oparesheni hiyo ni ya kwanza na kama watakamatwa kwa mara ya pili, watawafikisha mahakamani ili sheria nichukue mkondo wake.

No comments:

Post a Comment