18 September 2011

ATCL kuboresha huduma za anga

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL), limejipanga kukabiliana na changamoto walizonazo ili kuhakikisha linakuwa imara kama lilivyokuwa zamani. Mkakati huo umetangazwa
Dar es Salaam hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Bw. Paul Chizi, wakati akizungumzia maadhimisho wa miaka 50 ya uhuru na uhai wa shirika hilo.

Alisema shirika hilo linaangalia makosa yaliyojitokeza ili yaweze kurekebishwa na kufanya vizuri katika soko.

“Hivi sasa tumejipanga upya kuhakikisha shirika linakabiliana na ushindani uliopo ili tusiyumbe tena kama ilivyowahi kutokea, wafanyakazi watapewa mafunzo ya mara kwa mara ili kukabiliana na changamoto zilizopo na ushindani wa biashara.

“Tunapaswa kuwafurahisha wateja wetu bila hivyo hatuwezi kusonga mbele, ATCL inajipanga kuhakikisha tunalipa mishahara ya wafanyakazi sisi wenyewe badala ya kuitegemea Serikali,” alisema.

Alisema baada ya Serikali kuwapa mtaji, shirika litaanza kujitegemea ambapo Watanzania watalipenda hivyo wanaomba ushirikiano ili watoe huduma bora.

“Tumejipanga kumudu soko la ndani kwanza baada ya hapo, tutaangalia masoko ya nje, miaka mitatu ijayo ATCL itarudi katika hali ya kawaida kutokana na mikakati thabiti tuliyonayo, Watnzania wawe na imani kuwa shirika lao linarudi kwa kasi mpya,” alisema Bw. Chizi.

Aliongeza kuwa, ili kuhakikisha mikakati hiyo inafanikiwa na kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini, ndege ya shirika hilo aina ya DASH 8-300 iliyokuwa nchini Afrika Kusini kwa matengenezo, tayari imewasili.

Ndege hiyo iliwasili wiki iliyopita na wanatarajia hadi Septemba 25 mwaka huu, itakuwa imeanza safari za Tabora na Kigoma kila siku.

Alisema ndege nyingine ya DASH-8-300, wanatarajia kuifanyia matengenezo hpa nchini ili kuokoa gharama na muda kama  itapelekwa nje ya nchi.

Bw. Chiza aliongeza kuwa, tayari ATCL imeingia mkataba na kampuni ya Jetlink (T) Ltd, ili kupata ndege nyingine ambayo itatumika kwa dharula iwapo ndege za shirika hilo zitakuwa na tatizo.

Aliongeza kuwa, katika jitihada zake za kuboresha huduma za anga nchini, siku za usoni ATCL imepanga kukodi au kununua ndege zingine mbili aina ya CRJ 200 zenye uwezo wa kubeba abiria 50 kila moja kwa ajili ya soko la ndani.

Alisema baadaye shirika limepanga kuwa na ndege mbili aina ya CRJ/700 zenye uwezo wa kubeba abiria 70 kila moja ambazo zitasafari nchi jirani.

No comments:

Post a Comment