20 September 2011

Wabunge CHADEMA kortini Tabora

*Waachiwa kwa dhamana, kesi yao baada ya uchaguzi
*Warejea jimboni Igunga, wapokewa kwa maandamano


Moses Mabula na Benjamin Masese, Tabora

WABUNGE wawili na mjumbe wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA jana walifikishwa katika Mahakama ya
Mkoa wa Tabora wakikabiliwa na mashtaka manne ya kumshambulia na kumdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Fatuma Kimario.

Baada ya kesi yao kusomwa na kuachiwa kwa dhamana, walirejea wilayani Igunga kuendelea na kampeni, ambapo walipokewa na maandamano ya viongozi, mashabiki na wanachama wa chama hicho.

Wabunge hao ni Bw. Sylvester Kasulumbai, mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki na Suzan Kiwanga (Viti Maalumu) na Bw. Anwar Kashaga ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wijana Wilaya ya Igunga.

Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa wa Tabora, Bw. Thomas Simba, Mwendesha Mashtaka Bw. Juma Masanja, alidai kuwa mnamo Septemba 15, mwaka huu majira ya mchana katika Kijiji cha Isakamaliwa Kata ya Isakamaliwa wilaya Igunga, mshtakiwa wa kwanza Bw. Sylvester Kasulumbai alitoa Lugha ya matusi kwa Bi. Kimario.

Alidai kuwa mshtakiwa huyo alisema 'ni malaya mkubwa, huyu ndiye niliyetaka kuzaa naye, mpumbavu mkubwa an DC gani huyo hana akili'.

Aliongeza kuwa washitakiwa wote kwa pamoja walimshambulia Bi Kimario na kumsababishia maumivi ya kichwa.

Katika shtaka la tatu washitakiwa kwa pamoja walimshikilia Bi Kimario isipokuwa halali kinyume cha sheria.

Pia watuhumiwa hao walidaiwa kumwibia Bi Fatuma Kimario Simu ya mkononi aina ya Samsung yenye thamani ya sh. laki Nne 400,000. Walikana mashtaka hayo.

Masharti ya dhamana

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili wa chama hicho, Bw. Tundu Lisu akisaidiwa na wakili wa kujitegeme,a Bw Musa Kwikima, waliomba mahakama hiyo iwape dhamana washitakiwa kwa kuwa kosa hilo si kubwa na kwamba hawana shaka yoyote na hawezi kutoroka ukingatia washitakiwa wawili ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakili huyo wa CHADEMA aliomba mahakama kuwa ikiwezekana wabunge hao wajidhamini wenyewe kwani hawawezi kutoroka kutokana na nafasi waliyonayo katika bunge, lakini upande wa mashtaka ulikataa ombi la kujidhamini wenyewe bali wadhaminiwe.

Hakimu aliwaachiwa kwa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili kwa kiasi cha sh. milioni 5 ya kwa maneno, na wote walitimiza masharti yote ya dhamana na kuachiwa hadi Oktoba 10, mwaka huu kesi hiyo ikapotajwa tena.

Mahakama hiyo iliwaonya washitakiwa hao wasitende kosa lolote la jinai likalosababisha kufikishwa mahakamani katika kipindi chote cha kesi itapokuwa mahakamni, vinginevyo mahakama itafuta dhama yao.

Mapokezi yao Igunga

Maelfu ya wananchi wa Jimbo la Igunga walijitokeza kuwapokea viongozi hao wa CHADEMA katika Kata ya Ziba kilometa 29 kutoka Mjini Igunga, wakiwa wameongozana na wakili wao, Bw. Tindu Lissu ambaye ni Mkurugenzi wa sheria, Katiba na Haki za Binadamu.

Wabunge hao walifika Igunga saa 10 jioni na wananchi waliokuwa na magari, pikipiki, baiskeli, bajaj na waenda kwa miguu ambapo walichukua saa mbili kuandamana hadi kufika Igunga mjini

Maandamano hayo yaliyosababisha kusababisha barabara kuu ya Dar- Mwanza kuziba yaliwapa wakati mgumu polisi kuwapanga watu ili kuruhusu magari kupita na baadaye waliamua kukaa pembeni na kuangalia.

Baadhi mabango yaliyohusika katika maandamano hayo yalisomeka hivi 'bora ukimwi kuliko CCM, 'CCM wanamaliza kuni kwa kuchemsha mawe', Miaka 50 ya uhuru bila maji Igunga' na mengine.

Akizungumza na wananchi hao, Bw. Lissu aliwataka wananchi hasa vijana kutokuwa waoga katika kutetea haki yao pale wanapofanyiwa
hujuma bila kujali ni kiongozi wa serikali au mwanachama wa
chama chochote.

Alisema kuwa polisi walichofanya kwa kuwakamata viongozi hao watakijutia kwa sababu hawakutenda haki kwani mhalifu alikuwa ni DC Bi. Kimario.

Naye Bw. Kasulumbai alisema kukamatwa kwao kumewaongezea
umaarufu na nguvu ya kuwapambana na CCM 'hadi kieleweke'.

Alisema kuwa siku ya kupiga kura CHADEMA na wananchi hawatatoka katika maeneo ya vituo vya kupigia kura na watakaa hatua 20 kusubiri matokeo.

Alitoa mwito kwa serikali na wasimamizi wa uchaguzi huo
kuwa makini kwani wakijaribu kuchakachua wataadhibiwa
na nguvu ya umma na lazima CCM walie.

2 comments:

  1. Mbona kesi aliyofunguliwa DC Fatuma Kimario na CHADEMA ya kuvurunga mkutano wa CDM, Kukutwa na barua za maombi ya kusimamia zoezi la uchaguzi wakati DC sio tume ya uchaguzi (NEC) mbona kesi hiyo haijafikishwa mahakamani kama hii ya wabunge wa CDM.

    Tunataka kufahamu kama ma-DC wako juu ya sheria?

    Polisi msiwe jumuiya ya CCM fanyeni kazi yenu kwa haki, tunataka kumuona DC Fatuma akipelekwa naye Tabora mahakamani kujibu kesi inayomkabili. Vinginevyo POLISI mtakuwa mnachochea vurugu katika nchi hii kama wananchi wataona haki haitendeki.

    ReplyDelete
  2. Anonymous wewe ni shabiki wa chadema. Polisi hawawezi kupeleka kesi mahakamani kama haina ushahidi wa kosa la kueleweka. kosa la wabunge wa chadema lipo wazi.

    Haki au Mahakama haiendi kisiasa. Ingekua hivo hata wewe ungekamatwa kwa hoja ya uchochezi

    ReplyDelete