18 September 2011

UWAMATA wapinga kusitishwa safari za mabasi

Na Grace Ndosa

UMOJA wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA), umepinga kitendo cha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), kusitisha
safari za baadhi ya mabasi na umepanga kukutana na Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omari Nundu iliu kuzungumzia suala hilo.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa UWAMATA Bw. Salum Abdallah, alisema inashangaza SUMATRA kutumia nguvu kubwa ya kuyafungia mabasi badala ya kutafuta chanzo cha ajali ili waweze kuokoa maisha ya watu.

“Wiki iliyopita SUMATRA ilisitisha huduma za usafirishaji abiria kwa Kampuni ya mabasi ya Grazia kwa sababu ya kuhusika na ajali iliyosababisha vifo vya watu 10, Septemba 15 mwaka huu, eneo la  Mwidu, katikati ya Mdaula na Bwawani, mkoani Pwani.

“Pamoja na kusitisha huduma za mabasi ya kampuni hiyo, pia mamlaka hii imesitisha huduma za mabasi ya Sumry, Upendo, Morobest na Mohamed ili wayafanyie ukaguzi wa sifa, leseni za madereva wake na ubora wa mabasi hayo,” alisema.

Aliongeza kuwa, suala la vidhibiti mwendo limekuwa likizungumzwa kila siku lakini jambo la ajabu, inapotokea ajali na kuua, SUMATRA inakurupika na kusema wanataka kufanya uchunguzi wakati mabasi mengi hayajafungwa vifaa hivyo.

Alisema ajali inapotokea, mtu wa kwanza kulaumiwa ni dereva wakati SUMATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani wakijitoa katika lawama hizo wakati wao ndiyo wanaopaswa kubeba lawama kwa kushindwa kusimamia sheria zilizopo.

“Tayari tumemwandikia barua Bw. Nundu na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga, ili tuweze kukutana na kuzungumza.

No comments:

Post a Comment