Na Rabia Bakari
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Bw. Ezekiel Maige, amesema kukosekana kwa ndege za serikali ni kikwazo kimojawapo kikubwa katika ukuaji wa sekta ya
utalii nchini.
Pia Waziri Maige ametaja ajali ya meli ya Mv Spice Islanders iliyotokea Tanzania visiwani juzi kuwa ni pigo jingine kwa sekta ya utalii kwa kuwa imepeleka ujumbe mbaya kwa watalii kwamba Tanzania hakuna vyombo vya usafiri vya kuaminika.
Bw. Maige alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua warsha kuhusu mkakati na sera ili kukuza utalii inayojumuisha wajumbe kutoka Afrika Mashariki na Kusini iliyoandaliwa na Oganaizesheni ya Utalii ya Umoja wa Mataifa (UNWTO).
Alisema kukosekana kwa ndege za serikali zinazozunguka duniani kote kama ilivyo kwa nchi mbalimbali ni kikwazo kwa sekta ya utalii.
"Kukosekana kwa ndege za serikali za moja kwa moja, zinaathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu inachukua muda mwingi kwa watalii kuunganisha ndege, fedha na usumbufu hadi kufika nchini
Wengi wanaofika hapa wanatuambia kero hiyo, kwa kweli ni changamoto kwetu, kuwepo kwa ndege hizo si tu kubeba nembo ya Tanzania, pia inarahisisha watalii kufika moja kwa moja na kwa wingi, pia ni njia nyingine ya kutangaza nchi,"alisema Bw. Maige.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni bajeti finyu ya wizara hiyo ikilinganishwa na wapinzani wao katika sekta ya utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema kutokana na ufinyu wa bejeti wanakosa fedha ya kujitangaza, kukarabati maeneo yao ya vivutio ikiwemo miuundombinu.
Alisema licha ya changamoto hizo Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee ambavyo haviwezi kuingia katika ushindani na wengine na kwamba kinachohitajika ni kuvilinda kwa hali na mali.
Akizungumzia warsha hiyo Waziri Maige alitaja
lengo kuu kuwa ni kuboresha sera za utalii zilizopo pamoja na kupanga mikakati ya namna ya kuingia katika utalii wa pamoja Afrika Mashariki ili kusaidia kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii nchini.
"Pamoja na kuwa na mkakati wa kufanya utalii wa pamoja Afrika Mashariki, sisi Tanzania tutahakikisha tunaweka mawasiliano imara mipakani kuhakikisha watalii wanaoletwa na wenzetu wanahudumiwa na watu wetu na pia wanalala katika hoteli zetu ili sote tunufaike na utalii huo,"alisema Bw. Maige.
Katika hotuba yake Waziri Maige alitumia nafasi hiyo kuitangaza Tanzania ikiwemo hali ya hewa nzuri, mazingira pamoja na ukarimu wa watu wake.
Pia alitaja idadi ya watalii kuongezeka kutoka 501,669 hadi 782,699 katika kipindi cha mwaka jana pekee.
No comments:
Post a Comment