Na Zahoro Mlanzi
BAADA ya kutoka suluhu na Azam FC, timu ya Simba imekiri kuzidiwa ujanja na timu hiyo wakati zilipokutana katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara uliopigwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo zilikutana juzi ambapo licha ya matokeo hayo, mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba ilikwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 10, mbele ya JKT Ruvu ambayo ina pointi tisa.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo juzi, Ofisa Habari wa timu hiyo Ezekiel Kamwaga, alisema kiukweli walizidiwa ujanja kwani siku hazifanani lakini wanashukuru hawajapoteza mchezo wowote mpaka sasa.
"Tunamshukuru Mungu, tunaongoza ligi na pia tuna rekodi mpaka sasa hatujafungwa bao lolote na ikumbukwe kwamba kuondoka na pointi dhidi ya Azam, ambao walionekana kutuzidi ni jambo la kufurahia," alisema Kamwaga.
Alisema lengo lao ni kuondoka na pointi tatu, kama walivyofanya katika michezo mingine iliyotangulia, lakini hali haikuwa hivyo kwani timu waliyokutana nayo ilijiandaa vizuri na ndiyo maana wakagawana pointi.
Msemaji huyo alisema upungufu uliojitokeza katika mchezo huo ana uhakika Kocha Mkuu, Mosses Basena ameona na ataufanyia kazi na hivi sasa wanajiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Polisi Tanzania, ambao utapigwa Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji.
Naye Kocha Basena, akizungumzia suala la kumtoa kiungo wa pembeni, Shija Mkina muda mfupi baada ya kumwingiza, alisema hakuwa makini na mchezo baada ya kuoneshwa kadi ya njano.
Alisema unapomuaona mchezaji amehamaki ni dhahiri, kinachofuata ni kupewa kadi ya pili ya njano na baadaye nyekundu, hivyo ili kuepusha hilo ndiyo maana akaamua kumtoa na kumwingiza Uhuru Selemani.
Kitendo hicho kilizua maswali mengi miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo, ambao walihudhuria mchezo huo na kila mmoja alisema analolijua.
"Nilimwingiza Mkina, ili akaongeze mashambulizi baada ya awali kumtumia Kiemba, ambaye muda mwingi alikuwa akicheza eneo la katikati ambapo Mkina alipewa jukumu la kutanua uwanja na kupiga krosi ndani," alisema Basena.
No comments:
Post a Comment