21 September 2011

UHABA WA SUKARI

Pinda akerwa polisi kusindikiza magendo

*Awapa muda, vinginevyo JWTZ kuchukua hatamu
*Akemea ushabiki wa kisiasa unaovuruga amani


Na Grace Michael, Bunda

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amekasirishwa na taarifa kwamba Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mara linashiriki kuhujumu nchi kwa kusindikiza sukari kwenda nchi jirani, hivyo kulionya kuwa lisipojirekebisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) litaingilia kazi hiyo.

Alisema anawapa muda polisi kuhakikisha wanaachana na tabia hiyo vinginevyo serikali italiagiza JWTZ kuingilia kati ili kudhibiti utoroshaji wa sukari na kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo nchini.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bunda katika mkutano wa hadhara juzi, Bw. Pinda alisema serikali haiwezi kuvumumilia hali hiyo inayosababisha manung’uniko na kujenga dhana potofu kuwa serikali imeshindwa kazi.

““Nimepata pata taarifa kuwa sukari inayovushwa kimagendo kwenda nchi jirani wakati mwingine inasindikizwa na oolisi kwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu...kama mmeshindwa kazi yenu basi tutaliagiza jeshi liingilie kati,” alisema Bw. Pinda.

Aliwataka makamanda wa mikoa kukaa na askari wao kuona ni namna gani tabia hiyo inaachwa mara moja kwa kuwa inatia doa utendaji kazi wa serikali.

“Acheni tabia hii ya kushirikiana na wafanyabiashara ambao wao wanaangalia faida tu, tabia ya kusema kufa kufaana ni roho mbaya huwezi ukafanikisha uvushaji wa sukari ili wananchi waumie kwa ajili ya maslahi yao, tabia hii iachwe mara moja,” aliagiza Bw. Pinda huku akionyesha wazi kukerwa na suala hilo.

Aliutaka uongozi wa Wilaya ya Bunda kuhakikisha inawasaka wasambazaji wa bidhaa hiyo na endapo wataonekana kuhusika na hujuma hizo wanyang’anywe leseni mara moja ili kurejesha nidhamu ya wafanyabiashara.

Alisema pamoja na wafanyabiashara kuwa na mchango mkubwa kiuchumi lakini serikali haiwezi kuvumilia vitendo ambavyo inaona vinasababisha ugumu wa maisha kwa wananchi wake.

Akemea siasa za ushabiki

Bw. Pinda pia aliwataka wananchi na wanasiasa kuacha ushabiki wa kisiasa ambao unaweza kuondoa umoja na amani iliyopo kwa Watanzania.

Bw. Pinda aliyasema hayo juzi mjini Bunda na kuwataka wananchi kuwa makini na baadhi ya wanasiasa wanaobeza mambo yaliyofanywa na serikali katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru.

“Kuna tabia iliyojengeka ya kubeza kila jambo linalofanywa na serikali hata kama ni zuri kiasi gani, wanasiasa wanaofanya hivi lengo lao ni kupotosha wananchi ili waichukie serikali yao,” alisema.

Alisema ni vyema wananchi wakajenga utamaduni wa kushiriki katika siasa bila kuhatarisha amani na utulivu uliopo kwani gharama ya kurudisha amani iliyopotea ni kubwa.

“Tufanye yote lakini tuhakikishe hatuvunji umoja tulionao, kama serikali tumeweka demokrasia ya kutosha lakini isitumike vibaya, tulumbane lakini tusipigane na kama tuko kwenye uchaguzi tusemane lakini tusilipeleke taifa kubaya,” alisema Bw. Pinda.

“Kwa mfano, maisha yetu sisi tumeyazoea kulingana na tamaduni zetu, mtu wa kabila hili kaoa wa kabila jingine, mtu wa dini hii kaoa wa dini ile, mtu wa chama hiki anaishi na mtu wa chama kile, hivyo tuishi kwa misingi ya kulinda umoja wetu,” alisema.

No comments:

Post a Comment