21 September 2011

CUF wambebesha msalaba Msekwa

Na Peter Mwenda, Igunga

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemtupia lawama Makamu Mwenyekiti wa CCM (bara), Bw. Pius Msekwa kuwa endapo damu itamwagika katika uchaguzi mkdogo wa
Jimbo la Igunga ndiye atakuwa amesababisha.

Meneja Kampeni wa chama hicho Jimbo la Igunga, Bw. Antony Kayange akimnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Bw. Leopold Mahona katika kijiji cha Ncheli, Kata Sungwizi, alisema kitendo cha Bw. Msekwa kutangaza kuwa CCM itashinda katika jimbo hilo anataka damu imwagike.

Bw. Mayange alisema CCM haina chake kwa sababu imekuwa ikitaka
wananchi wa Igunga wachague mbunge wa chama hicho lakini akichaguliwa haonekani tena mpaka uchaguzi mwingine uje, huku akiacha wananchi wakiendelea kuteseka kwa shida zilizokithiri.

Bw. Pius Msekwa alikaririwa akitamba kwenye vyombo vya habari kuwa pamoja ya matukio ya hapa na pale yanayofanywa na vyama vya upinzani, bado CCM itashinda katika uchaguzi wa mbunge utakaofanyika Oktoba 2, mwaka huu.

Kampeni za chama hicho zilizofanyika juzi katika Tarafa ya Simbo
alikozaliwa na kusoma Bw. Mahona, watu waliohudhuria kumsikiliza walimtaka asiige tabia za wabunge waliopita wa CCM pindi wanapochaguliwa hukimbilia Dar es Salaam wao wakibaki yatima na hawana sehemu ya kupeleka matatizo yao.

“Nimedhamiria kuokoa maisha ya ndugu zangu wa Igunga, ndiyo maana mwaka jana nilibaki peke yangu nikiomba kura zenu kwa baiskeli. Kati ya wagombea 13 waliochukua fomu za Ubunge nikapambana na mbunge aliyejiuzulu CCM hivi karibuni, Bw. Rostam Aziz na nikashinda vishawishi vyake vya kutaka nijitoe nikang’angana hadi mwisho nikashika nafasi ya pili nikipata kura 11,000,” alisema Bw. Mahona.

Kampeni za CUF zilitarajiwa kuendelea jana katika vijiji 96 vya Jimbo la Igunga ambalo wananchi wake wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji ya safi ya kunywa na  kunywesha mifugo yao.

“Huyu Pius Msekwa anatangaza CCM itachukua jimbo hili yaani wasukuma na wanyamwezi wote hatuwezi kudanganywa kama walivyozoea kufanya wanavyotaka,” alisema Bw. Mahona.

Mikakati ya kampeni

Akizungumzian kampeni za uchaguzi wa Igunga, Naibu katibu Mkuu wa CUF (Bara), Bw. Julius Mtatiro alisema wamejipanga vizuri na kuongeza timu kufikia 6 na kufanya mikutano 36 kwa siku katika kata 26 za Igunga.

Alisema baada wabunge sita wa Zanzibar kuwasili wengine 10 wanatarajia kuwasili leo, wengine 15 Alhamisi, na Ijumaa
wataongezeka watano na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Bw. Mtatiro alisema timu hiyo inaongeza mikutano kufikia 45 kwa siku na kutamba kuwa chama chake kiko tayari kupiga kampeni ya chini kwa chini, juu kwa juu na miguu kwa miguu.

Alisema vyama vingine vikileta helkopta moja, CUF nayo inafanya hivyo hivyo, vikileta tatu na hata kumi nacho kitafanya hivyo mpaka jimbo hilo libaki kwa chama hicho.

5 comments:

  1. Huyu Pius Msekwa hana jipya ni fisadi ambaye ameifilisi Ngorongoro kwa kutumia kivuli cha Makamu Mwenyekiti wa CCM na Mwenyekiti wa Bodi. Wana Igunga si wajinga kumsikiliza huyu anayetakiwa naye kujivua gamba. Watu wameshazeeka mpaka mboni za macho zimeshakutana lakini hawataki kung'atuka ama kweli CCM inaficha mafisadi. Katika kujivua gamba mbona huyu hawamshughulikii? Rostam hakuwa peke yake wenzake vipi mbona wanaendelea kudunda? Ama kweli CCM ni kichaka maalum cha mafisadi ndio maana mafisadi na majambazi wote wanajiunga CCM ili kujificha huko.

    ReplyDelete
  2. tuendeshe kampeni zetu kwa ustaharabu ili tuwape wananchi nafasi ya kumchagua mgombea wanayemtaka

    ReplyDelete
  3. Wananchi tumechoka na wanasiasa wanaoomba kura, wakipata wanahamia mijini, WanaIgunga chaguaeni mbunge atakayewafaa msikubalikurubuniwa kwa vijisenti uchwara vya hao wanasiasa twala. Pembueni mchele na pumba.

    ReplyDelete
  4. Kweli Mfa Maji Haachi kutapatapa. CUF CUF hivi kwa mtaji gani mpaka Mshinde Jimbo hili, Lenye Kata 35 Madiwani 35 ambapo Madiwani 3 Chadema, 32 CCM . CUF 0 SAU 0 hata ukiwa kipofu lakini kwa Upofu wa Akili wanajiona wapo sawa tu. Ningelikuwa mimi hata ukucha siuweki hadharani kwa Mtaji gani nilionao? Nijuavyo na Nionavyo Mimi Mpiga kura Trh 2/10/2011 ni CCM, CCM. Wavaa Magwanda hatuwahitaji Mkoani kwetu:

    ReplyDelete
  5. WW unaejiita mwana ccm ww ndio juha wa kutupa.CCM imefanya nini igunga? mbona shida ya maji iko palepale kwa muda wa Miaka 50.Je? unasemaje kwa hilo?
    Mh.Rostam mlichaguwa kwa wingi wa kura,matokeo uliayaona sina haja ya kuyarudia tena.
    Kwa maoni yangu ninaomba ukapimwe akili yako labda imeharibika kutokana na mihadarati uliokuwa ukiitumia hapo awali.

    ReplyDelete