14 September 2011

TFF yapandisha viingilio Chamazi

Na Zahoro Mlanzi

VIINGILIO vya michezo ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Chamazi uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, vimepanda kutoka 5,000 kwa mzunguko,  mpaka
sh. 7,000 na Viti Maalum sh. 20,000, badala ya 15,000, ili kudhibiti uingiaji wa watu uwanjani.

Mbali na hilo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limebaini kwamba, uwanja huo una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000, badala 7,000 kama walivyoambiwa awali na uongozi unaomiliki uwanja huo.

Akizungumza Dar es Salam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema wamelazimika kupunguza baada ya kugundua kuwa, uwanja huo una uwezo wa kuchukua watu 5,000 na kwamba, viingilio vya awali havitaweza kukidhi tija ya uwanja, kwani watu watakuwa wengi kuliko mahitaji ya uwanja.

"Baada ya kupewa taarifa hizo,  tukaona ni bora tujiridhishe wenyewe, ambapo tulituma watu wakaukagua uwanja na wakaleta ripoti kwamba, ni watu 5,000 tu, ndio watakaoingia uwanjani, hivyo viingilio tulivyoweka ni dhahiri watu watakuwa wengi sana," alisema Wambura na kuongeza;

"Tukaona ni bora tuweke viingilio vya sh. 7,000 na sh. 20,000,  ambapo tunajua watu watakuwa si wengi na usalama utakuwepo kwa kiwango kizuri, kama mnavyojua uwanja haujakamilika na mpango wao baadaye uingize watu zaidi ya idadi hiyo," alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo na uwanja upo nje ya mji, wanawaomba mashabiki wa timu hizo, kununua tiketi katika vituo vya Shule ya Sekondari ya Benjamini Mkapa, Oil Com  Ubungo na Mbagala Rangitatu,  mbali na vituo hivyo, tiketi hazitapatikana.

Alisema wamefanya hivyo ili kila shabiki anayekwenda huko, awe na tiketi kabisa ili kuondoa adha ya kukosa tiketi uwanjani na kupoteza nauli yake, hivyo ana  imani atakayekosa tiketi mjini, hatakwenda Chamazi.

1 comment:

  1. TFF siku zote wanawaza pesa na sio watazamaji pamoja na kukuza soka nasema hivi kwa sababu wange weza kuuza hizo tiketi kwa utaratibu walio usema na kuhakikisha tiketi zitakazo uzwa katika vituo walivyochagua haziuzwi zaidi ya tiketi 5,000.Hii inamaana wapenzi wa soka wasio na vipato vikubwa hawataweza kuona baathi ya michezo kwa sababu ya ukiritimba wa TFF.

    ReplyDelete